KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 2, 2011

Stars kuanza kambi leo

TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars inatarajiwa kuingia kambini leo kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wake wa michuano ya awali ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad.
Taifa Stars na Chad zinatarajiwa kumenyana Novemba 11 mwaka huu mjini Nd’jamena kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana ilieleza kuwa, wachezaji wanatakiwa kuripoti kambini leo, isipokuwa wale wanaocheza soka ya kulipwa nje, ambao wataanza kuingia kambini keshokutwa.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema, kambi ya Taifa Stars itakuwa kwenye hoteli ya New Africa na mazoezi yatafanyika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Wambura alisema, timu hiyo inatarajiwa kwenda N’Djamena Novemba 8 mwaka huu.
Alisema waamuzi waliopangwa kuchezesha mechi hiyo wanatoka nchini Nigeria. Liwataja waamuzi hao kuwa ni Bunmi Ogunkolade, Tunde Abidoye, Baba Abel na Abubakar Ago.
Mtathimini wa waamuzi atakuwa Idrissa Sarr kutoka Mauritania wakati kamishna wa mchezo huo ni Hamid Haddadj kutoka Algeria.
Wachezaji walioteuliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ni makipa Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ally (Azam).
Wengine ni Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya), Erasto Nyoni (Azam), Nadir Haroub (Yanga) na Godfrey Taita wa Yanga.
Wachezaji wengine ni Juma Jabu (Simba), Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Nurdin Bakari (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Ramadhan Chombo (Azam) na Shomari Kapombe (Simba). Wakali wengine ni Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu(TP Mazembe, DR Congo), Dan Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden), na Hussein Javu (Mtibwa Sugar).

No comments:

Post a Comment