'
Wednesday, November 9, 2011
ROSE NDAUKA: Wasambazaji wameikwamisha filamu yangu
MTAYARISHAJI na muigizaji nyota wa Bongo, Rose Ndauka amesema, ameshindwa kuiingiza sokono filamu yake mpya ya The Diary kutokana na matatizo ya usambazaji.
Badala yake, Rose amesema ameamua kuiingiza sokoni filamu yake nyingine mpya ya Ruben n’ Angel wakati akipiga hesabu juu ya nini la kufanya kuhusu The Diary.
Rose alisema hayo mjini Dar es Salaam wiki hii, alipokuwa akijibu swali kuhusu kuchelewa kuingia sokoni kwa filamu yake hiyo, iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki.
Mwanadada huyo amecheza filamu ya The Diary kwa kushirikiana na Wema Sepetu na Jacqueline Pentzel ‘Jack wa Chuzi’.
“Kuna matatizo yametokea kuhusu usambazaji. Yule msambazaji wa awali ameshindwa kufanyakazi hiyo, hivyo kwa sasa nasubiri kuangalia nini la kufanya,”alisema.
Filamu ya The Diary ilikuwa itoke mapema mwaka huu, ikiwa imetengenezwa na Kampuni ya Jarowe. Filamu hiyo ilikuwa ianze kuingia sokono kabla ya filamu ya Ruben n’ Angel.
Hata hivyo, kampuni ya Jarowe haikudumu kutokana na wasanii hao watatu kushindwa kuelewana huku filamu yao ya The Diary ikihamishwa kutoka msambazaji mmoja hadi mwingine.
Rose amekuwa akitayarisha filamu zake mwenyewe kupitia kampuni yake ya Rose Ndauka Entertainment ya mjini Dar es Salaam. Pia amekuwa akishiriki kucheza filamu za kampuni nyingine.
Mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema, anatarajia kumtangaza msambazaji mpya wa filamu hiyo hivi karibuni.
“Nilikuwa nimewaahidi wapenzi wa kazi zangu kuwa, filamu ya The Diary inatoka mwezi huu, na watu walikuwa wakisubiri kazi yangu kwa hamu itoke, lakini ratiba imebadilika, “alisema Rose.
“Badala yake nimetoa filamu nyingine ya Ruben n’ Angel, ambayo nayo ni kali na ya kusisimua, kwa sababu nina wapenda watu wangu, nimewaletea filamu ya ukweli, baadae ndiyo itafuatia filamu ya The Diary,” aliongeza.
Nyota ya Rose ilianza kung’ara alipokuwa katika kundi la Bulls Entertainment, ambako alishiriki kucheza filamu ya Swahiba na kufanikiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa fani hiyo.
Filamu hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Rose kushiriki kuicheza tangu alipojitosa katika fani hiyo, ikifuatiwa na filamu ya Bad Girl.
Pamoja na kupata mafanikio makubwa katika kazi yake ya uigizaji, Ndauka anakiri kuwa suala la kumpata mume haliwezi kuwa mikononi mwake kutokana na uhusiano wake na wanaume kushindwa kudumu.
“Ni muda mrefu sasa nimetamani kuolewa ili nianzishe familia yangu, lakini sasa nimeamini ndoa anapanga Mungu, ndio maana nimeamua kumuachia yeye aniletee mume pale muda wangu utakapofika,”alisema.
Alisema akiwa mwanamke anayejitegemea, amejitosheleza kwa kila la kitu, lakini kwenye suala la ndoa, ameamua kumwachia Mungu.
Rose alisema hawezi kujiamulia ni lini ataolewa kwa sababu yupo kwenye subira na uamuzi wa kuoa huwa ni wa mwanaume.
Mwaka jana, Rose ambaye anapenda kuolewa na mwanaume mchapakazi, alitangaza kuchumbiwa, lakini baadaye ilidaiwa kuwa, aliyemvisha pete alikuwa mume wa mtu.
Akizungumzia tasnia ya filamu nchini, Rose alikiri kwamba, imetawaliwa na matukio mengi ya ushirikina kwa lengo la wasanii kutaka kujipatia umaarufu na wengine kuzima nyota za wenzao.
Filamu zingine maarufu, ambazo Rose ameshiriki kuzicheza ni pamoja na My Dreams, Kipuli, More than Pain na Deception.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
This comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDelete