KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 9, 2011

Yondani aota mbawa Yanga



UONGOZI wa klabu ya Simba umemalizana na beki wake mahiri, Kevin Yondani na kufikia makubaliano ya kuendelea kuichezea timu hiyo msimu ujao.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, beki huyo alifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa juu wa klabu hiyo wiki iliyopita na kufikia uamuzi wa kumaliza tofauti kati yao.
Kwa mujibu wa habari hizo, mazungumzo hayo yalikwenda vizuri na Yondani amekubali kuendelea kuichezea timu hiyo msimu ujao.
Yondani aligoma kuripoti kwenye kambi ya timu hiyo kwa wiki kadhaa kwa kile kilichodaiwa kuwa, hajamaliziwa fedha zake za usajili.
Kugoma kwa Yondani kujiunga na Simba, kulizusha hisia kuwa, huenda akajiunga na mahasimu wao Yanga wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wa kamati ya usajili ya Yanga walikaririwa jana wakisema kuwa, hawawezi kulipa fedha nyingi kwa ajili ya kumsajili beki huyo, badala yake watasubiri mkataba wake Simba umalizike.
Mkataba wa Yondani kuichezea Simba unatarajiwa kumalizika baada ya msimu huu na uongozi wa klabu hiyo umekaririwa ukisema kuwa, upo tayari kumuuza kwa dola 100,000 za Marekani (sh. milioni 17).
“Tatizo la Yondani limeshamalizika, tutakuwa naye katika mzunguko wa pili wa ligi kuu na upo uwezekano mkubwa akaendelea kuwa na Simba msimu ujao,” alisema kiongozi mmoja wa juu wa Simba alipozungumza na Burudani jana.
Hata hivyo, kiongozi huyo alikiri kuwa, bado Yondani hajajibu barua aliyoandikiwa ya kumtaka aeleze sababu za kushindwa kujiunga na timu hiyo wakati wa ligi.
“Ni kweli aliandikiwa barua na kukabidhiwa mkononi, lakini hadi ninapozungumza na wewe hivi sasa, hajajibu barua hiyo. Lakini nilicho na uhakika nacho ni kwamba, ameshamalizana na uongozi na tutaendelea kuwa naye msimu ujao,”alisema kiongozi huyo.
Wakati huo huo, Simba imesema itatangaza majina ya wachezaji wake watakaoachwa wakati wa usajili wa dirisha dogo baada ya kujadili ripoti ya Kocha Moses Basena.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kuwa, ripoti ya kocha huyo, haikuweza kujadiliwa katika kikao cha kamati ya utendaji wiki iliyopita kutokana na kufiwa na mama yake mzazi.
Kamwaga alisema, mara baada ya Basena kurejea nchini, kamati ya utendaji itakutana kwa dharula kujadili ripoti yake kabla ya kutangaza majina ya wachezaji hao.
Basena ndiye aliyepewa jukumu la kupendekeza majina ya wachezaji watakaoachwa na wale wapya watakaosajiliwa wakati wa dirisha dogo.
Tayari Simba imeshatangaza kumwacha kiungo wake, Jerry Santo, aliyepata timu barani Asia na nafasi yake itachukuliwa na Derreck Walulya. Klabu hiyo pia imetangaza kuwa, itawapandisha daraja wachezaji wanne wa kikosi cha pili.

No comments:

Post a Comment