KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, July 19, 2014

TAIFA STARS MIKONONI MWA MAMBA WA MSUMBIJI KESHO, KIINGILIO BUKU SABA




Viingilio kwa mechi ya Taifa Stars na Msumbiji itakayochezwa keshokutwa (Jumapili) Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ni sh. 7,000 na sh. 30,000 kwa viti maalumu 4,500 tu.

Kuanzia kesho asubuhi (Jumamosi) tiketi za kielektroniki zitauzwa pia katika magari maalumu kwenye vituo vya Buguruni Shell, Dar Live Mbagala, Ferry Magogoni, Kigamboni, OilCom Chang’ombe, OilCom Ubungo, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa (Kariakoo), TCC Club Chang’ombe na Uwanja wa Taifa.

Aidha tiketi zinapatikana kupitia M-PESA kwa kupiga *150*00# kisha bonyeza 4, bonyeza tena 4 kisha weka namba ya kampuni 173399 kisha ingiza 7000 kama namba ya kumbukumbu ya malipo, kisha andika tena 7000 kwenye weka kiasi, kasha weka namba ya siri na baadaye bonyeza 1 kukubali.

Utapokea ujumbe wenye orodha ya vituo vya MaxMalipo vya kuchukua tiketi ukiwa na namba ya uhakiki wa malipo yako.

Vituo vya MaxMalipo vya kuchukulia tiketi ni mgahawa wa Steers uliopo mtaa wa Samora/Ohio, maduka makubwa ya Uchumi Supermarket (Quality Centre, Tabata Segerea na kituo cha daladala Makumbusho), Sheer Illussions (Millennium Tower na Mlimani City), maduka makubwa ya TSN Supermarket (City Centre, Kibo Tegeta na Upanga).

Vodashop (Ubungo na Mill Pamba), Shop Mwenge (Born to Shine), Puma Petrol Station (Mwenge na Uwanja wa Ndege), Engen Petrol Station (Mbezi Beach), Big Bon Petrol Station (Kariakoo, Sinza Mori, Mbagala na Temeke), YMCA (Posta Mpya), City Sports Lounge (Posta), Uwanja wa Taifa) na Uwanja wa Karume.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Msumbiji hatua za awali Kombe la Mataifa ya Afika (AFCON).

Nooij ambaye amewahi kuifundisha Msumbiji amesema katika Mkutano na Waandishi wa Habari hoteli ya Coutyard, eneo la Sea View, Dar es Salaam kwamba wachezaji wake wote wapo fiti kwa mchezo huo.

“Nafahamu sana mchezo utakuwa mgumu, hii ni timu yangu na timu yenu pia, naamini mshindi ni yule ambaye atacheza kitimu zaidi Jumapili,”amesema.

Amesikitika kiungo Jonas Mkude ameshindwa kuhusika na mchezo wa Jumapili kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, hata hivyo amesema ana matumaini mchezaji huyo wa Simba anaweza kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

Ametaja kikosi alichoteua kwa ajili ya mchezo wa kesho, kuwa ni makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Aishi Manula, mabeki Said Mourad, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Aggrey Morris, Kevin Yondan na Edward Charles, wakati viungo ni Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Shaaban Nditi, Simon Msuva, Himid Mao, Mwinyi Kazimoto, Khamis Mcha, Ramadhani Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo, Amri Kiemba na washambuliaji Mrisho Ngassa, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na John Bocco,

Kwa upande wake, Nahodha wa Taifa Stars Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kwamba anaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi Uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam kuisapoti timu yao.

“Tunashukuru hadi kufika hapa, ni matunda ya kupambana kwa juhudi na pia sapoti yenu, kwa hivyo tunaomba muendelee kuwa nasi Jumapili, watu waje kwa wingi wasapoti timu, ifanya vizuri,”amesema Cannavaro.

Aidha nahodha huyo wa taifa Stars amesema bado ana kumbukumbu za kipigo walichokipata dhidi ya Msumbiji mwaka 2007,wakati Nooij akiwa kocha mkuu wa Mambas, na kwa maana hiyo hivi sasa akiwa chini yake atafanya kila juhudi kwa faida ya Watanzania na yeye mwenyewe binafsi.

Stars itamenyana na Msumbiji Jumapili katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya AFCON mwakani nchini Morocco, ambao kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 7,000.

Stars ilifika hatua hii baada ya kuitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 1-0 Dar es Salaam na kwenda kulazimisha sare ya 2-2 Harare.

Timu itakayofuzu hatua hii itaingia kwenye Kundi C ambalo lina timu za Zambia, Cerpe Verde na Niger zilizofuzu moja kwa moja hatua hiyo, kuwania tiketi ya Morocco mwakani.

Katika kuwania tiketi ya AFCON ya mwaka jana nchini Afrika Kusini, Tanzania ilitolewa na Msumbiji kwa penalti 5-4 baada ya sare ya jumla ya 2-2 Dar es Salaam na Maputo, Stars ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen.

Stars inaonekana kuwa na maandalizi mazuri safari hii chini Mholanzi, Nooi na uongozi mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Rais Jamal Malinzi.

Baada ya kuitoa Zimbabwe, wachezaji walipata mapumziko ya wiki moja, kabla ya kwenda Botswana kuweka kambi ya wiki, na waliporejea Mbeya kuweka kambi ya wiki moja na ushei.

Nchini Botswana, pamoja na mazoezi, pia Stars ilipata mechi tatu za kujipima nguvu, ambazo

walifungwa mbili, moja dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Botswana mabao 4-2 na nyingine dhidi ya timu ya jeshi la nchini humo, BDF walishinda moja 3-1 na kufungwa moja 2-1.

Tanzania imewahi kushiriki mara moja tu AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilitolewa katika hatua ya makundi, ilipokuwa pamoja na wenyeji Nigeria, Ivory Coast na Misri, Kundi A. Ilifungwa 3-0 na Nigeria, 2-1 na Misri na kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast.

No comments:

Post a Comment