KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, July 18, 2014

SERENGETI BOYS MIKONONI MWA AFRIKA KUSINI LEO



TIMU ya soka ya Taifa ya vijana wa chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys inashuka dimbani leo kumenyana na Afrika Kusini katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Shelisheli na kiingilio kitakuwa sh. 2,000.

Waamuzi hao ambao waliwasili nchini juzi usiku kwa ndege ya Kenya Airways ni Allister Barra, Gerard Pool, Jean Joseph Felix Ernest na Nelson Emile Fred.

Kamishna wa mechi hiyo Andriamiasasoa Doda Nirimboavonjy kutoka Madagascar pia ameshawasili.

Afrika Kusini (Amajimbos) ilitua nchini juzi ikiwa na msafara wa watu 37 na imefikia hoteli ya Sapphire. Amajimbos ilifanya mazoezi jana jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Kikosi cha Serengeti Boys chini ya kocha Hababuu Ali Omari kipo kambini kwa zaidi ya wiki mbili sasa kikijiandaa kwa mechi hiyo. Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 nchini Afrika Kusini.

Wakati huo huo, Alfred Kishongole Rwiza wa Tanzania ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya marudiano ya michuano hiyo ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Rwanda na Uganda.

Mechi hiyo itachezwa nchini Rwanda kati ya Agosti 1 na 3 mwaka huu. Waamuzi wa mechi hiyo watatoka Burundi wakiongozwa na Pacifique Ndabihawenimana.

No comments:

Post a Comment