'
Wednesday, July 2, 2014
STARS YAJIPIMA NA BOTSWANA
Timu ya Taifa (Taifa Stars) inacheza mechi ya kirafiki na Botswana leo (Julai Mosi
mwaka huu) kuanzia saa 9 alasiri kwa saa za huko.
Mechi itakayofanyika Uwanja wa Taifa jijini Gaborone ni sehemu ya maandalizi ya Taifa
Stars kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji (Mambas)
itakayochezwa Julai 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inatarajiwa kurejea nchini Julai 6
mwaka huu kuendelea na programu nyingine kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji.
Wakati huo huo, kutakuwa na utaratibu maalumu kwa waandishi wa habari za michezo
kwa ajili ya kuripoti mechi ya Stars dhidi ya Msumbiji. Hivyo, vyombo vya habari
vinatakiwa kutuma majina mawili ya waandishi watakaoripoti mechi hiyo. Mwisho wa
kupokea majina hayo ni Julai 8 mwaka huu.
WACHEZAJI WATANO WAOMBEWA ITC
Wachezaji watano wameombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) ili waweze
kucheza mpira wa miguu nchini na nje ya Tanzania.
Abdulhalim Humoud kutoka Simba, Crispine Odulla (Coastal Union) na Haji Ugando
(Mbagala Market FC) wameombewa ITC na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya
(FKF) ili wakacheze nchini humo katika klabu za Sofapaka, Bandari FC na Nakuru All
Stars.
Vilevile TFF imemuombea ITC mchezaji Ismaila Diarra kutoka nchini Mali ili aweze
kujiunga na timu ya Azam FC. TFF inafanyia kazi maombi hayo, na mara taratibu zote
zitakapokamilika itatoa ITC hizo kwa wachezaji wanaokwenda nje ya Tanzania.
SERENGETI BOYS YAJINOA KUIKABILI AFRIKA KUSINI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea vizuri
na mazoezi kujiandaa kwa mechi ya mashindano dhidi ya Afrika Kusini (Amajimbos).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itachezwa Ijumaa ya Julai 18 mwaka huu Uwanja
wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari ameshafanya mchujo wa awali wa
wachezaji wa timu hiyo kutoka 39 na kubaki na 31. Timu hiyo imepiga kambi kwenye
hosteli ya TFF iliyopo Uwanja wa Karume.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment