MCHEZA filamu nyota wa kike nchini, Jacqueline Wolper amesema baadhi ya watu wanampiga vita kwa sababu ya chuki walizonazo dhidi yake.
Jacqueline amesema watu hao wamekuwa wakimzushia kashfa mbalimbali kwa lengo la kumpaka matope na pia kumchonganisha na wasanii wenzake.
Mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema hayo mwanzoni mwa wiki hii, kufuatia kuenea kwa uvumi amepokonywa gari lake aina ya BMW X6 na mwanaume aliyekuwa amemzawadia.
Jacqueline alisema uvumi huo hauna ukweli wowote kwa sababu bado anamiliki gari hilo na kwamba si kweli kuwa amenyang’anywa.
“Kuna dada mmoja, ambaye amekuwa akieneza habari za uzushi kuhusu mimi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa ninakosana na wasanii wezangu, “alisema msanii huyo.
“Hivi karibuni nikiwa location (sehemu ya kuchezea filamu), rafiki zangu walinipigia simu wakinijulisha kuwa kuna habari zinatangazwa katika redio na baadhi ya mitandao kwamba nimenyang’anywa gari langu, habari ambazo si za kweli kwa sababu gari langu lipo ndani nyumbani kwangu,”alisema Jacqueline akionekana kuwa na uchungu.
Msanii huyo aliyecheza filamu zaidi ya 20 alisema kama ni suala la magari, anayo mengi na hakuna mtu wa kumpangia atembee na lipi na kwa siku ipi.
Jacqueline alisema anao ushahidi kwamba uvumi huo umekuwa ukienezwa na mtangazaji mmoja wa kike, lakini hakutaka kumtaja kwa madai kuwa, akisoma taarifa hizi atajitambua.
No comments:
Post a Comment