UONGOZI wa klabu ya Coastal Union ya Tanga umeanza kufanya mazungumzo na beki Derrick Walulya wa URA ya Uganda kwa ajili ya kumsajili msimu ujao wa ligi.
Kiongozi mmoja wa Coastal Union, ambaye hakuenda jina lake litajwe gazetini, alithibitisha jana kufanyika kwa mazungumzo hayo na kuongeza kuwa bado hawajafikia mwafaka.
Walulya ni mmoja wa wachezaji waliong’ara katika kikosi cha URA kinachoshiriki katika michuano ya Kombe la Kagame, inayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Beki huyo alisajiliwa na Simba msimu uliopita, lakini hakuweza kuichezea mechi nyingi kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Uongozi wa Simba uliamua kumwacha Walulya kwenye usajili wa msimu ujao kwa madai ya kushuka kwa kiwango chake kabla ya mchezaji huyo kuibukia URA.
Walulya alikuwa kikwazo kikubwa kwa washambuliaji wa Simba wakati timu hizo zilipomenyana katika mechi za hatua ya makundi. Katika mechi hiyo, URA iliichapa Simba mabao 2-0.
Mbali na Walulya, Coastal Union pia ilikuwa ikifanya mipango ya kumsajili kiungo wa zamani wa Simba, Jerry Santo ambaye alikuwepo kwenye kikosi cha Tusker ya Kenya.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Coastal Union, iwapo mazungumzo kati yao na Walulya yatakwenda vizuri, beki huyo huenda akavaa jezi za klabu hiyo msimu ujao.
No comments:
Post a Comment