KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

Okwi azua balaa Simba

KUZAGAA kwa taarifa za mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba kusajiliwa na Yanga kumesababisha tafrani kubwa miongoni mwa wanachama wa klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.
Tangu iliporipotiwa na gazeti moja la michezo wiki iliyopita kuwa Okwi amesajiliwa na Yanga, wanachama na mashabiki wa Simba hawana raha na wamekuwa wakihoji iweje viongozi wao wamuuze kwa mahasimu wao.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ hivi karibuni alijikuta akionja joto ya jiwe baada ya kuzingirwa na mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wakitaka waelezwe iwapo ni kweli Okwi amesajiliwa na Yanga.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari wiki iliyopita, Kaburu alikana mchezaji huyo kusajiliwa na Yanga na kuweka bayana kwa vyombo vya habari mkataba wa mchezaji huyo, ambao utamalizika mwaka 2013.
Mbali na kuonyesha mkataba huo kwa waandishi wa habari, Kaburu alizungumza moja kwa moja kwa njia ya simu na Okwi akiwa mjini Kampala, Uganda, ambapo alimuhakikishia kuwa, hajafanya kitu kama hicho.
Okwi alimueleza Kaburu kwamba, alikuwa akishughulikia viza ya kumwezesha kwenda Italia kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Parma na kwamba iwapo atakwama, atarejea Simba.
Licha ya uthibitisho huo kutoka kwa Okwi, baadhi ya viongozi wa Yanga wanadaiwa kuwa, wamekuwa wakiwahakikishia wanachama wao kwamba wamefanikiwa kumsajili mchezaji huyo na kwamba wanachosubiri ni kumalizana na Simba.
Kwa mujibu wa kanuni za usajili, Yanga haiwezi kumsajili Okwi bila kuzungumza na Simba kwa vile bado ana mkataba na klabu hiyo na kama zitafikia makubaliano, Yanga italazimika kulipa gharama za kuvunja mkataba.
Katika kudhihirisha kwamba taarifa hizo zimekuwa zikiwakera mashabiki na wanachama wa Simba, juzi waliweka ulinzi mkali kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Yanga ilipokuwa ikicheza mechi ya kirafiki na JKT Ruvu.
Wakati wa mechi hiyo, wanachama wa Simba maarufu kwa jina la makomandoo, waliweka ulinzi mkali katika milango ya kuingilia jukwaa kuu ili kuhakikisha kuwa, mchezaji huyo hawezi kuingia uwanjani.
Hofu ya makomandoo hao wa Simba ilitokana na taarifa zilizotolewa na kiongozi mmoja wa Yanga kwamba, wangemtambulisha Okwi na mchezaji mwingine mpya wakati wa mechi hiyo.
Hata hivyo, ulinzi huo ulionekana kuwa ni wa bure kwa vile hakukuwepo na uwezekano wa Okwi kufika uwanjani akiwa ameongozana na viongozi wa Yanga.
Kiongozi mmoja wa Yanga, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini aliieleza Burudani jana kuwa, klabu yake haina mpango wowote wa kumsajili mchezaji huyo na wanashangazwa na uvumi huo, ambao umekuwa ukienezwa na vyombo vya habari.
“Hizi habari hata sisi zinatushangaza kwa sababu taratibu za usajili zipo wazi, tukitaka kumsajili Okwi lazima kwanza tuzungumze na Simba na kukubaliana kuvunja mkataba wake,”alisema.
Naye kiongozi mmoja mwandamizi wa Simba, ambaye hakutaka atajwe gazetini aliwataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wazipuuze habari hizo kwa sababu hazina ukweli wowote.
“Huu ni uvumi tu usiokuwa na maana yoyote kwa sababu Yanga haina uwezo wa kumsajili Okwi na mwenyewe amesema akishindwa majaribio Italia, atarudi Simba,”alisema.

No comments:

Post a Comment