MWIGIZAJI nyota wa filamu nchini, Zuwena Mohamed 'Shilole' amesema tangu alipojitosa kwenye fani ya muziki, baadhi ya waigizaji wenzake wameanza kufuata nyayo zake.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Shilole alisema alichokifanya ni kama kuwafungulia njia ya kujiongezea kipato wasanii wenzake japokuwa baadhi yao hawana vipaji vya muziki.
"Kila mwigizaji kwa sasa anataka kuimba na kuwa mwanamuziki, japokuwa wengi hawana uwezo huo. Wanapoona Shilole anakata viuno stejini, wanajua kila msanii ataweza kufanya hivyo,"alisema Shilole, ambaye amejipatia sifa nyingi kutokana na kucheza filamu mbalimbali.
Shilole alisema binafsi hakujitosa kwenye fani hiyo kwa kukurupuka ama kubahatisha, bali ni baada ya kufanya tathmini ya kina na kubaini kwamba ana kipaji cha fani hiyo.
“Nawapa pole wenzangu, tangu nimefungua njia na kuanza kuimba, naona wanakurupuka na kuingia katika fani ya uimbaji. Mimi sikukurupuka, nilijipanga kwa ajili ya kazi na inaonekana,"alisema Shilole.
"Napata maonyesho mengi, ambayo hata wasanii wakubwa hawapati. Mimi si kama hawa wakataa viuno wanaoiga baada ya kumuona Shilole. Sifanyi maigizo, nafanya kazi inayokubalika katika jamii,”aliongeza.
Kutokana na kushiriki kwake kwenye fani ya filamu na muziki, Shilole alisema kwa sasa amekuwa na uwezo wa kuwasomesha watoto wake wawili katika shule za kimataifa na pia anamiliki gari zuri na la kifahari. Pia alisema anaishi kwenye nyumba nzuri.
Shilole ameshakamilisha baadhi ya nyimbo zake za muziki wa kizazi kipya, akiwashirikisha Mzee Yusuf (Kachumbari), Barnaba (Surprise), Q Chilla (Dudu) na wimbo wa Viuno, aliowashirikisha wasanii Richi Mavoko na Kitokololo.
Mwanadada huyo pia anamiliki kampuni yake binafsi, inayojulikana kwa jina la Shilole Classic, ambayo inasimamia kazi zake zote za muziki na filamu.
No comments:
Post a Comment