KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 19, 2012

MANJI ASEMA KAZI IMEANZA, KUSAJILI NYOTA WAWILI WA KIMATAIFA

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji amesema ana deni kubwa kwa wanachama wa klabu hiyo na atalazimika kurejesha fadhila kwao.
Manji alisema hayo mjini Dar es Salaam jana katika mahojiano maalumu na gazeti la Burudani.
Alisema yeye na viongozi wenzake wapya wa Yanga wameshaanza kutekeleza majukumu yao na matunda yake yalianza kuonekana juzi wakati timu hiyo ilipomenyana na Wau Salaam ya Sudan Kusini.
Manji alikuwa miongoni mwa viongozi wapya wa Yanga walioshuhudia mechi hiyo, akiwa ameketi kwenye kiti maalumu uwanjani, nyuma ya benchi la wachezaji wa akiba wa timu hiyo.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliibamiza Wau Salaam mabao 7-1 na kuweka hai matumaini ya kufuzu kucheza robo fainali.
Manji amewashukuru wanachama wote wa Yanga walioshiriki kwenye uchaguzi mdogo wa klabu hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwataka wampe ushirikiano.
“Nawashukuru wanachama wote walioshiriki kupiga kura katika uchaguzi huo pamoja na kamati ya uchaguzi kwa kusimamia vyema mchakato wa utoaji fomu hadi upigaji kura,”alisema.
Manji alisema kushinda kwake kwa kishindo katika uchaguzi huo ni ishara njema kwamba wanachama wa Yanga wanamkubali, kumuamini na kuridhishwa na uwezo wake.
Mwenyekiti huyo pia alivipongeza vyombo vya habari kwa kuripoti vizuri na kwa umakini mchakato wote wa uchaguzi na kuongeza kuwa, amepanga kukutana navyo kwa lengo la kuvishukuru baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Kagame.
Amewataka wanachama pamoja na wajumbe wa baraza la wazee wa Yanga kuwapa ushirikiano yeye na viongozi wenzake wapya ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao.
“Tunapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, kusiwe na makundi tena ndani ya Yanga kwa sababu makundi yalishavunjika baada ya uchaguzi,”alisema.
Manji alisema bila ya kuwepo kwa ushirikiano miongoni mwa wanachama na viongozi, itakuwa vigumu kwa Yanga kupata mafanikio katika michuano yoyote itakayoshiriki.
Mwenyekiti huyo alisema pia kuwa, ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake katika mechi dhidi ya Wau Salaam iliyochezwa juzi na kuongeza kuwa, walistahili kupata ushindi huo mkubwa.
Alisema aliamua kutazama mechi hiyo akiwa chini ya uwanja badala ya jukwaa kuu ili kufuatilia kwa makini mawasiliano kati ya benchi la ufundi na wachezaji.
Manji alisema amefurahishwa na usajili wa wachezaji wapya uliofanywa na mjumbe wa kamati ya utendaji, Abdalla Bin Kleb na makamu mwenyekiti wa kamati ya usajili, Seif Ahmed kwa vile ni mzuri.
Alisema kazi iliyobaki ni kwa wachezaji hao kuonyesha uwezo wao kwa kucheza kwa ari na kujituma kwa lengo la kuiletea Yanga mafanikio.

No comments:

Post a Comment