“Maisha Plus 2012 litakuwa shindano la kipekee na lenye uwezo wa kumjengea stadi nzuri kijana kwa kuwa lina mambo mengi mapya na tofauti na ilivyozoeleka,’’anasema mwasisi wa shindani hilo, Masoud Ally, maarufu zaidi kwa jina la Kipanya.
Kipanya alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akizungumzia kuhusu ujio mpya wa shindano la Maisha Plus 2012, ambalo limefanyiwa mabadiliko makubwa ili kukidhi kiu ya watanzania na kumuinua kijana katika maisha yake ya kila siku.
Hii ni kwa sababu moja ya masharti na vigezo kwa mshiriki wa Maisha Plus mwaka huu ni kuwa na ujuzi wa ziada utakaomuwezesha kuwa katika nafasi nzuri ya kuibuka mshindi wa shindano hilo.
Kipanya, ambaye ni mratibu wa shindano hilo alisema, Maisha Plus ni shindano lenye dhima ya kumuandaa kijana kwa maisha ya baadaye na kwa mwaka huu wamekuja na mambo mengi mapya.
“Tunataka kuona kijana anathamini chakula pamoja na mwanamke anayekiandaa kwa kuwa wanawake wengi ndio wazalishaji chakula, hivyo uwepo wa vijana ndani ya kijiji utawafanya wawe mabalozi wazuri juu ya chakula,’’alisema.
Kwa mujibu wa Kipanya, shindano la mwaka huu litakuwa na mambo mengi mapya ikiwa ni pamoja na washiriki wa Maisha Plus kuishi ndani ya kijiji pamoja na akina mama 14 waliopatikana katika shindano la Mama Shujaa wa Chakula.
Kipanya alisema kina mama hao wamepatikana katika shindano hilo linalodhaminiwa na Taasisi ya OXFAM, ambayo ni miongoni mwa wadhamini wa Maisha Plus mwaka huu.
“Utofauti wa shindano la mwaka huu ni ushiriki wa akina mama ndani ya kijiji, ambao watakaa kwa siku 14, ikiwa ni siku tatu kabla ya washiriki wa Maisha Plus hawajawasili ndani ya kijiji,’’alisema.
Kipanya alisema baada ya kuwasili washiriki 36 wa Maisha Plus, watakaa pamoja na akina mama hao kwa siku tatu na kufanya kazi mbalimbali za kijiji, kabla ya washiriki 10 na akina mama hao kuondoka.
“Watatoka washiriki 10 pamoja akina mama watakaokuwepo ndani ya kijiji na kubaki washiriki 26 watakaoanza safari ya miezi miwili ya shindano la Maisha Plus, ambayo hatimaye mtamwezesha mshindi kuondoka na sh. milioni 20,’’alisema.
Kipanya alisema Maisha Plus ni shindano linalozungumzia maisha ya kijijini, hivyo washiriki 26 watakaobaki watakuwa wanafanya kazi mbali mbali za kijiji, lengo likiwa kumjenga na kumuelimisha juu ya kukihifadhi na kukiheshimu chakula.
‘Vijana wengi hivi sasa hawaheshimu chakula, hasa kutokana na kutojua wapi kinapotoka, hivyo Maisha Plus ya mwaka huu itakuwa darasa tosha kwa mashabiki wake,’’alisema.
Kipanya alisema anaamini shindano hilo litaibua ari na nidhamu kubwa kwa vijana katika kuheshimu na kuwa mstari wa mbele katika kuzalisha chakula kijijini.
“Watalima mazao mbalimbali, ambayo yatakuwa sehemu ya chakula chao kipindi chote watakachokuwemo ndani ya kijiji, hivyo watakuwa na stadi muhimu katika maisha yao,’’ alisema.
Kipanya alisema Maisha Plus na Mama Shujaa wa Chakula ni mpango wa pamoja wenye kuwawezesha wanawake na vijana katika uzalishaji wa chakula na kusaidia kutekeleza mipango yao mbali mbali ya kujikwamua kiuchumi.
Alisema usaili wa shindano la Maisha Plus unatarajiwa kuanza Agosti Mosi mwaka huu katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na Visiwani ili kupata washiriki wa shindano hilo.Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Morogoro, Tanga, Dodoma, Arusha, Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya, Iringa, Mwanza, Tabora na Zanzibar.
“Mikoa mingine tutaitangaza baadaye, lakini hiyo ni ya kwanza na tutaanza na Arusha katika wiki ya kwanza ya mwezi Agosti,’’alisema.
Katika usaili huo, Kipanya alisema wataangalia vigezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na umri kuanzia miaka 21 hadi 26, awe mbunifu, raia wa Tanzania na kuweza kuwasiliana vyema na wenzake ndani ya kijiji.
Kutokana na yote hayo, Kipanya alisema ujio wa shindano hilo ni mageuzi mapya ya Maisha Plus kwa kuwa vijana watafaidika na kuwa wenye ujuzi zaidi kutokana na uelewa watakaoupata ndani ya kijiji kwa miezi miwili watakayoishi.
No comments:
Post a Comment