MABINGWA watetezi wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame, Yanga leo watakuwa na kibarua kingine kigumu watakapomenyana na Mafunzo ya Zanzibar katika mechi ya robo fainali itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga imefuzu kucheza hatua hiyo baada ya kushika nafasi ya pili katika kundi C nyuma ya Atletico ya Burundi wakati Mafunzo imeshika nafasi ya kwanza katika kundi B.
Katika mechi nyingine ya robo fainali itakayochezwa kesho kuanzia saa nane mchana, URA ya Uganda itavaana na APR ya Rwanda.
Mechi zote mbili zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa vile kila timu itapania kushinda ili kusonga mbele na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Yanga huenda ikashuka dimbani bila ya mshambuliaji wake nyota, Saidi Bahanuzi na kiungo Nizar Khalfan kutokana na kuwa majeruhi.
Daktari wa Yanga, Muhidin Sufiani alisema jana kuwa, Bahanuzi anasumbuliwa na maumivu ya mgongo wakati Nizar anasumbuliwa na nyonga.
Sufiani aliwataja wachezaji wengine wanaoumwa kuwa ni kipa Yaw Berko, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ na mshambuliaji Hamisi Kiiza.
Hata hivyo, Sufiani alisema hali za wachezaji hao zinaendelea vizuri na upo uwezekano mkubwa wa kushuka dimbani kucheza mechi ya leo.
Daktari huyo alisema sababu za wachezaji hao kuumia mara kwa mara ni kucheza mechi mfulilizo tangu mashindano hayo yalipoanza Julai 14 mwaka huu na hivyo kukosa muda wa kupumzika.
Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet alisema hataweza kuwatumia wachezaji wengine zaidi ya 20 waliosajiliwa kwa ajili ya kombe hilo hivyo hana la kufanya zaidi ya kupambana na hali hiyo.
Tom alisema amemwagiza Sufiani kufanya kila linalowezekana ili Kiiza, Chuji na Berko waweze kucheza mechi hiyo, lakini alikiri kuwa, hilo halitawezekana kwa Nizar kutokana na ukubwa wa tatizo linalomsumbua.
Bahanuzi ndiye kinara wa kufunga mabao kwa Yanga hadi sasa, akiwa amepachika wavuni mabao manne na ni mmoja wa wachezaji wanaowania tuzo ya mfungaji bora.
Hata hivyo, iwapo Bahanuzi atashindwa kushuka dimbani, pengo lake huenda likazibwa na Jerry Tegete wakati nafasi ya Nizar upo uwezekano mkubwa ikachukuliwa na Juma Seif ‘Kijiko’.
Pambano kati ya URA na APR pia linatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi kutokana na staili ya uchezaji ya timu hizo na pia kuundwa na wachezaji wengi nyota.
Ilitwaa imetinga robo fainali baada ya kuongoza kundi A wakati APR ilishika nafasi ya tatu katika kundi C.
Kocha Mkuu wa URA, Alex Isabirye alisema juzi kuwa, lengo lao kubwa mwaka huu ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa michuano hiyo.
URA ilishiriki michuano hiyo kwa mara ya mwisho mwaka 2010 nchini Uganda, ambapo ilitolewa hatua ya makundi.
RATIBA ROBO FAINALI
Julai 23, 2012 URA vs APR (Saa 8:00 mchana)
Mafunzo vs Yanga (Saa 10:00 jioni)
Julai 24, Atletico vs AS Vita (Saa 8:00 mchana)
Azam vs Simba SC (Saa 10:000 jioni)
No comments:
Post a Comment