KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 26, 2012

YANGA, AZAM USO KWA USO FAINALI YA KOMBE LA KAGAME

Mshambuliaji Hamisi Kiiza (kulia) wa Yanga akijiandaa kumtoka beki wa APR ya Rwanda wakati wa pambano lao la leo.


Mshambuliaji Kipre Tchetche (kulia) wa Azam akitafuta mbinu za kumtoka beki wa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.


Yanga na Azam leo zimefuzu kucheza fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Kagame baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya APR ya Rwanda na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Katika mechi hizo za nusu fainali zilizochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliichapa APR bao 1-0 wakati Azam iliicharaza AS Vita mabao 2-1.

Mshambuliaji Mrisho Ngasa aliibuka shujaa wa Azam baada ya kuifungia bao la pili katika kipindi cha pili na kwenda kushangilia bao hilo kwenye jukwaa la mashabiki wa Yanga, ambao awali walikuwa wakiwazomea wachezaji wa Azam.

Katika kudhihirisha mapenzi yake kwa Yanga, mara baada ya mchezo huo kumalizika, Ngasa badala ya kupongezana na wachezaji wenzake wa Azam, alikwenda tena kwenye jukwaa la mashabiki wa klabu hiyo, ambao walimshangilia na kumkabidhi jezi ya njano, ambayo aliipokea na kutokomea nayo jukwaani.

Pambano kati ya Yanga na APR lilikuwa na upinzani mkali kutokana na timu zote mbili kucheza kwa kukamiana na hivyo kulifanya liwe gumu kutabirika.

Ilibidi Yanga isubiri hadi dakika 30 za nyongeza kupata bao hilo pekee na la ushindi baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.

Uzembe wa mabeki wawili wa APR kuzozana na mchezaji mmoja wa Yanga, aliyeangushwa chini ndio uliosababisha kupatikana kwa bao hilo.

Rashid Gumbo, aliyeingia kipindi cha pili alitumia fursa hiyo kurusha mpira kwa haraka, ukamkuta Haruna Niyonzima, aliyemimina krosi golini, ikamkuta Hamisi Kiiza, aliyeunganisha wavuni kwa kifua.

Bao hilo lilipokewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa Yanga, ambao muda mwingi wa mchezo huo walikuwa kimya kutokana na kutoamini iwapo timu yao ingeibuka na ushindi.

Kwa matokeo hayo, Yanga na Azam sasa zitakutana katika fainali ya michuano hiyo itakayopigwa Jumamosi kuanzia saa 10 jioni.

Mechi hiyo itatanguliwa na ile ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya APR na AS Vita itakayopigwa kuanzia saa nane mchana.Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa kitita cha dola 30,000, wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000.

No comments:

Post a Comment