KLABU ya Yanga mwishoni mwa wiki hii inatarajiwa kufanya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi sita za uongozi zilizowazi utakaofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa michezo nchini ni ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji.
Uchaguzi huo umeitishwa kutokana na kujiuzulu kwa mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, makamu wake, Davis Mosha na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji kutokana na sababu mbalimbali.
Wajumbe wa kamati ya utendaji waliotangaza kujiuzulu ni Seif Ahmed, Ally Mayay, Edgar Chibula na Abdallah Bin Kleb wakati Theonest Rutashoborwa alifariki dunia.
Kujiuzulu kwa baadhi ya viongozi hao, hasa Nchunga kulitokana na kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutakiwa wawajibike baada ya Yanga kuchapwa mabao 5-0 na Simba katika mechi ya mwisho ya michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hizo za uongozi ni Yussuf Manji, Edgar Chibula na John Jambele wanaowania nafasi ya mwenyekiti. Wengine ni Ayoub Nyenzi, Stanley Kevela na Clement Sanga wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti.
Wanaowania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ni Lameck Nyambaya, Mohamed Mbaraka, Ramadhan Saidi, Edgar Fongo, Beda Tindwa na George Manyama. Wengine ni Aaron Nyanda, Omary Ndula,Jumanne Mwamenywa, Abdallah Binkleb, Peter Haule, Justine Baruti, Gaudencius Ishengoma na Kevela.
Tayari wagombea wote waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hizo za uongozi na kupitishwa na kamati ya uchaguzi ya Yanga na ile ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wameshaanza kampeni kwa ajili ya kunadi sera zao kwa wanachama.
Wagombea hao wamekuwa wakipita kwenye matawi mbalimbali ya wanachama yaliyopo mjini Dar es Salaam wakielezea mikakati yao ya uongozi na mbinu watakazotumia katika kuikwamua klabu hiyo ili iondokane na matatizo ya kifedha na utegemezi wa wafadhili.
Miongoni mwa watu waliofanikisha kuitishwa kwa uchaguzi huo ni Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Yanga, Jaji John Mkwawa, ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo miaka mitatu iliyopita.
Jaji Mkwawa ndiye aliyesimamia usaili wa wagombea, usikilizaji wa pingamizi zilizowekwa na baadhi ya wanachama na pia ndiye atakayeongoza mkutano wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumapili.
Wakati wagombea wakiwa kwenye kampeni, Jaji Mkwawa ametoa tahadhari kwa wanachama wa klabu hiyo, akiwataka wawe makini katika kusikiliza sera za wagombea na hatimaye kuchagua viongozi wenye sifa na uwezo.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Jaji Mkwawa alisema wanachama wa Yanga wanapaswa kuepuka makosa waliyoyafanya katika uchaguzi uliopita kwa kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuiletea maendeleo klabu hiyo.
Jaji Mkwawa alisema kutokana na klabu hiyo kupitia katika misukosuko mingi ya uongozi, wakati sasa umefika kwa wanachama kuanza kuona mbali na kutorudia makosa ya miaka ya nyuma.
Aliyataja baadhi ya mabadiliko yanayotakiwa kufanyika ndani ya Yanga kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mabadiliko ya utawala na uendeshaji wa klabu hiyo.
“Utaratibu wa uongozi katika klabu ya Yanga umepitwa na wakati na unapaswa kuachwa mara moja. Tunatakiwa kuwa na viongozi wenye fani, ikiwa ni pamoja na utawala wa soka,”alisema Jaji Mkwawa.
Alisema Yanga inatakiwa kuwa na viongozi watakaoweza kusimamia vyema raslimali za klabu hiyo, yakiwemo majengo na uwanja wa soka wa Kaunda ili iweze kujiendesha kibiashara na kuacha kuwategemea wafadhili.
Jaji Mkwawa alisema utaratibu wa sasa wa kuiendesha Yanga kwa kutegemea misaada ya wafadhili na mapato ya mechi za ligi umepitwa na wakati na haustahili kuendelea kupewa nafasi.
Alisema jengo la Yanga lililopo mtaa wa Mafia na makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam ni raslimali tosha za kuiwezesha klabu hiyo kupata mapato mengi na kujiendesha kibiashara.
Jaji huyo alisema pia kuwa, uwanja wa Kaunda ukitengenezwa vizuri na kutumika kwa mazoezi, mechi za kirafiki na za ligi, nao unaweza kuiingizia Yanga mapato mengi na kuifanya ijitegemee.
“Mimi naamini wanachama wa Yanga wanawajua vyema wagombea waliojitokeza kuwania uongozi na wenye uwezo wa kubadili mfumo wa sasa wa uendeshaji wake kuwa wa kampuni ili ijiendesha kibiashara,”alisema.
Jaji Mkwawa alivitaja vyanzo vingine vya mapato, ambavyo vikitumiwa vyema vinaweza kuikwamua Yanga kuwa ni pamoja na uuzaji wa fulana, kofia na bidhaa zingine zenye nembo ya klabu hiyo.
Alisema kwa sasa biashara hiyo inafanyika holela bila ya kuinufaisha klabu hiyo zaidi ya wajanja wachache, ambao wamekuwa wakitumia mapato yatokanayo na biashara hiyo kujinufaisha.
Ametoa mwito kwa viongozi wapya watakaopatikana katika uchaguzi wa Jumapili kuandikisha wanachama wapya katika mikoa yote nchini ili ada za uanachama ziweze kutumika kuiendesha klabu hiyo kibiashara.
Alisema klabu ya Yanga inao uwezo wa kuandikisha wanachama zaidi ya milioni 10 nchi nzima na iwapo wote watalipa ada zao kila mwaka, fedha zitakazopatikana zitakuwa na manufaa makubwa kwa klabu.
Ametoa mwito kwa viongozi wapya wa Yanga kutambua vyema majukumu yao na changamoto zilizo mbele yao ili klabu hiyo iweze kusonga mbele kimaendeleo badala ya kurudi nyuma ama kudumaa.
"Napenda kuiona Yanga ikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi, ni lazima wanachama wabadilike kwa kuchagua viongozi imara,"alisema Jaji Mkwawa.
Jaji huyo pia ametaka kuundwa kwa sheria kali zitakazowazuia wanachama wa klabu hiyo na nyinginezo nchini kukimbilia mahakamani badala ya kwenye vyombo vingine kuwasilisha malalamiko yanayohusu mchezo huo.
Alisema utaratibu wa kufikisha masuala ya soka mahakamani umepitwa na wakati na umekuwa ukichangia kudumaza maendeleo ya mchezo huo kwa vile kesi za aina hiyo huchukua muda mrefu kusikilizwa.
“Sheria ipo wazi kwa FIFA (Shirikisho la Soka la Dunia) na kinachotakiwa ni utekelezaji tu kwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na klabu za soka,”alisema.
No comments:
Post a Comment