MBUNGE wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto (CHADEMA), amezilipua kampuni za simu nchini kwa kuwanyonya watanzania hasa wasanii wa muziki kutokana na kuingiza mamilioni ya shilingi na kuwalipa kiduchu.
Amesema kampuni hizo ikiwemo Vodacom na Airtel zimekuwa zikiingiza kiasi cha sh. bilioni 43 kwa mwaka kwa kupitia Kampuni ya On Mobile kutokana na tozo za miito ya simu ambayo ni kazi za wasanii nchini. Pia amesema kuwa kampuni hiyo haijasajiliwa hivyo inaendesha shughuli zake kinyume cha taratibu na kutaka hatua zichukuliwe.
Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma, alilipua bomu hilo bungeni jana wakati akichangia hotuba ya makadirio ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, ambapo alisema huo ni wizi na unyonyaji kwa watanzania.
Alisema kampuni hizo hutoza sh. 400 kwa siku kwa kutumia nyimbo hizo za miito na sh.37 kila unapotumia miito hiyo, lakini msanii wa Tanzania amekuwa akiambulia asilimia saba ya mapato hayo huku kampuni hizo zikichukua asilimia 80 na asilimia 13 inakwenda kwa Kampuni ya On Mobile.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimpigia Waziri Mkuu utasikia muito ya simu wa nyimbo ya Rose Mhando, ukimpigia Malima utasikia wimbo wa Dar mpaka Moro na ukinipigia mimi aidha utasikia nyimbo ya Chadema au kidumu, lakini wasanii hawa hawalipwi ipasavyo,
“Inashangaza Mheshimiwa Mwenyekiti kampuni hii ya Oo Mobile haina leseni ya kufanya kazi hiyo, imejibana kati ya makampuni hayo tu na ina watumishi wawili tu, lakini inachukua fedha nyingi huku wasanii wetu wakibaki masikini, hii haiwezekani", alisema Zitto.
Alisema hakuna sababu ya kuendelea kuwepo kwa kampuni hiyo iliyojibanza kati ya VodaCom na Airtel inayojulikana kwa jina hilo la On Mobile, hivyo iondolewe kwani inafanya biashara bila leseni na kulikosesha taifa mapato.
Mbunge huyo alisema serikali inapaswa kusimama kuwatetea wasanii hao kwani kampuni hizo za simu ni kubwa hivyo ni rahisi kuwakandamiza.
Alisema wakati umefika sasa kwa kampuni hizo, ambazo zinatumia nyimbo za wasanii kama muito katika simu zao ni bora wakamlipa msanii mtunzi asilimia 50 ya mapato yanayotokana na kutumia nyimbo hizo.
Aidha Zitto alipendekeza kutumika kwa Shirika la Posta Tanzania katika kusambaza kazi za wasanii nchini badala ya wasambazaji wa kawaida wa sasa ambao wamekuwa wakiwaibia wasanii.
Mbunge huyo alisema shirika hilo lipo katika maeneo mengi na hasa maeneo ya vijijini na kwa sasa halina kazi nyingi hivyo serikali iliongeze na shirika hilo ili kuokoa kazi za wasanii.
No comments:
Post a Comment