KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

KAGERE AIBANIA YANGA

MSHAMBULIAJI wa timu ya soka ya Polisi ya Rwanda, Meddie Kagere ameondoka nchini baada ya kukutana na viongozi wa kamati ya usajili ya klabu ya Yanga.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seif Ahmed alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wameshindwa kufikia makubaliano na Kagere kuhusu usajili wake.
Seif alisema walipanga kumsajili Kagere kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, lakini mchezaji huyo ametaka alipwe kiasi kikubwa cha fedha, ambacho wameshindwa kumpatia.
Kwa mujibu wa Seif, Kagere aliondoka nchini juzi kwa ndege kurejea Rwanda.
Hata hivyo, Seif alisema wanatarajia kukutana tena na mchezaji huyo wiki ijayo ili kuendelea na mazungumzo yao. Alisema lengo lao ni kuhakikisha wananasa saini ya mshambuliaji huyo.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, Kagere ameshindwa kukubaliana na kamati hiyo baada ya wakala wake kutoka Serbia kutaka dau kubwa.
Nyota huyo binafsi alikuwa tayari kuingia mkataba na Yanga, lakini wakala huyo alitaka kulipwa pesa nyingi hali iliyosababisha mazungumzo hayo kukwama.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Kagere na wakala wake wameahidi kujadiliana suala hilo wakiwa Rwanda kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.
Habari zimeeleza kuwa, iwapo Kagere atashindwa kurejea nchini, kamati ya usajili imepanga kuongeza mshambuliaji mwingine kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame, inayotarajiwa kuanza keshokutwa.

No comments:

Post a Comment