MSANII nyota wa vichekesho wa kundi la Vituko Show, Mussa Yusuph ‘Kitale’ ameamua kujiunga na kundi la muziki wa kizazi kipya la Mtanashaji.
Meneja wa kundi hilo, Maneno Tozz alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, Kitale amejiunga na Mtanashati kwa lengo la kuendeleza kipaji chake cha muziki.
Maneno alisema mbali na fani ya vichekesho na uigizaji wa filamu, Kitale ni msanii mahiri wa muziki na tayari ameshatunga wimbo mmoja.
Aliwataja wasanii wengine wanaounda kundi hilo kuwa ni Dogo Janja, PNC, Amazon na Happy. Alisema kundi hilo linamilikiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mtanashati Entertainment, Ustaadh Juma Namusoma.
“Lengo letu ni kuwa na kundi la mfano wa kuigwa na makundi mengine,”alisema.
Maneno alisema kundi hilo linaundwa na wasanii wengi nyota, ambao wapo chini ya PNC, ambaye kwa sasa anatamba kwa kibao chake kipya cha Binadamu na dunia.
Alisema wameamua kumchukua Dogo Janja kwa lengo la kuendeleza kipaji chake baada ya kukorofishana na uongozi wa kundi la Tip Top Connection.
Licha ya kumchukua msanii huyo, Maneno alisema watahakikisha anaendelea na masomo yake katika shule ya sekondari ya Makongo kwa kuwa elimu ni muhimu zaidi kwake kuliko muziki.
“Lengo letu ni kuona msanii huyu anasoma kwa sababu fani ya muziki ni sawa na Big G, lakini akiwa na elimu yake, maisha yake yataweza kuwa mazuri,”alisema.
Alisema kundi hilo si la mabishoo ama mabitozi kama baadhi ya watu wanavyopenda kuliita, bali ni la wasanii wenye vipaji vya muziki na waliodhamiria kuonyesha maajabu.
No comments:
Post a Comment