Ngasa akianza kuvaa jezi yenye rangi ya kijani na njano aliyopewa na mashabiki wa Yanga wakati Azam ilipokuwa ikimenyana na AS Vita ya DRC.
Ngasa akivaa jezi ya Yanga aliyopewa na mashabiki wa tawi la Yanga Bomba wakati Azam ilipomenyana na AS Vita ya DRC wakati wa mechi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame Ngasa akielekea kwenye mlango wa kuingia uwanjani baada ya kuvaa jezi ya Yanga (Picha zote na Emmanuel Ndege wa blogu ya liwazozito)
Mshambuliaji Mrisho Ngasa juzi alifanya vitendo vya ajabu wakati timu yake ya Azam ilipokuwa ikimenyana na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Kagame.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Ngasa aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche.
Kituko chake cha kwanza ni kwenda kushangilia bao la pili aliloifungua Azam katika mechi hiyo kwenye jukwaa wanalokaa mashabiki wa Yanga.
Muda wote wa pambano hilo, mashabiki hao walikuwa wakiizomea Azam, lakini baada ya mchezaji huyo kufunga bao na kuwafuata, walianza kumshangilia kwa mayowe mengi.
Kama hiyo haikutosha, mara baada ya pambano hilo kumalizika, Ngasa alikwenda kuungana na wachezaji wenzake kushangilia ushindi, badala yake alikwenda tena kwenye jukwaa la mashabiki wa Yanga, ambao walizidi kumshangilia.
Mbali na kumshangilia, mashabiki hao wa tawi la Yanga Bomba, walimzawadia Ngasa jezi yenye rangi ya kijani na njano, ambayo aliipokea na kuivaa mara moja na kisha kutokomea nayo nje ya uwanja, akipitia mlango maalumu wa dharula, mahali linapoegeshwa gari la wagonjwa.
Wakati Ngasa akitokomea nje ya uwanja, wachezaji wenzake pamoja na viongozi waliunda duara uwanjani wakiomba dua na kumshukuru Mungu kwa kuweza kushinda pambano hilo.
Mmoja wa maofisa wa Azam, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alikiri kuwa, uongozi umekerwa na kitendo hicho cha Ngasa na huenda ukamchukulia hatua za kinidhamu.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Ngasa tangu michuano ya Kombe la Kagame ilipoanza wiki mbili zilizopita.
Kocha Stewart Hall hakuwa anamchezesha kwa madai kwamba, alikuwa hajitumi mazoezini na kuonyesha dalili za kutaka kucheza.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wamekielezea kitendo hicho cha Ngasa kuwa kilikuwa ishara ya kumwonyesha Stewart kwamba uwezo wake bado upo juu.
Wengine wamekitafsiri kuwa, kilikuwa ishara ya kuitaka Azam imruhusu arejee Yanga, timu aliyoichezea kwa miaka kadhaa kabla ya kununuliwa na wana rambaramba kwa kitita cha zaidi ya sh. milioni 50.
No comments:
Post a Comment