KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema kutolewa
mapema kwa timu yake katika michuano ya Kombe la Kagame
kumechangiwa na maandalizi hafifu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya timu hiyo
kuchapwa mabao 3-1 na Azam juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, kocha huyo alisema Simba haikufanya maandalizi ya
kutosha kabla ya kushiriki michuano hiyo.
Milovan alikiri kuwa kikosi chake bado dhaifu kutokana na
kuundwa na wachezaji wengi wapya na pia wachezaji wake bado
hawajaweza kucheza kwa uelewano mkubwa.
Alisema alishalibaini tatizo hilo kabla hata ya kuanza kwa
michuano ya Kombe la Kagame na alishawaeleza mapema
viongozi wa klabu hiyo.
“Bado sina kikosi kizuri, ambacho unaweza kujivunia wakati
unashiriki katika michuano migumu kama hii," alisema.
Milovan alisema licha ya timu yake kutwaa ubingwa wa Kombe la
Urafiki kwa kuifunga Azam kwa njia ya penalti, bado hajaweza
kuunda kikosi imara na chenye ushindani.
“Lazima timu ipate maandalizi ya kutosha kabla ya kushiriki
mashindano makubwa kama haya. Kwa muda, ambao Simba
imejiandaa, tusingeweza kufika mbali,”alisema.
Aliimwagia sifa Azam kwa kusema ni timu nzuri na wachezaji
wake wanacheza kwa uelewano mkubwa kutokana na kukaa
pamoja kwa muda mrefu.
Hata hivyo, kocha huyo alisema ataendelea kukiimarisha kikosi
chake kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa ligi na kuhakikisha
wanatetea taji lao. Ligi hiyo imepangwa kuanza Septemba mwaka
huu.
No comments:
Post a Comment