KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

MILOVAN: SIMBA IPO KAMILI KILA IDARA

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema kikosi chake kwa sasa kimekamilika baada ya timu hiyo kushiriki katika michuano ya Kombe la Urafiki visiwani Zanzibar.
Akizungumza na Burudani mjini hapa juzi, Milovan alisema ushiriki wa Simba katika michuano hiyo umemsaidia kujenga kikosi imara na kinachocheza kwa uelewano mkubwa.
Kocha huyo kutoka Serbia alisema michuano hiyo imewasaidia wachezaji wake wapya kuelewana na wale wa zamani na pia kupata kikosi cha kwanza.
Aliwasifu wachezaji wote wapya waliosajiliwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuwa ni wazuri na wana vipaji vya hali ya juu vya kusakata kabumbu.
Milovan alisema ana hakika kikosi chake kitafanya vizuri katika michuano ya Kombe la Kagame, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Sitazami tu michuano ya Kombe la Kagame, lengo letu ni kufanya vizuri katika michuano ijayo ya ligi na kimataifa,”alisema kocha huyo, anayesifika kwa kufundisha soka ya kitabuni.
Kwa upande wake, kipa Juma Kaseja amewataka mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi kwa vile kikosi chao kimekamilika na kimepania kuonyesha maajabu kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
Alisema ushiriki wao katika michuano ya Kombe la Kagame umesaidia kuwajenga wachezaji na kuifanya timu icheze kwa uelewano mkubwa.
Kiungo mpya wa timu hiyo, Kanu Mbiyavanga alisema anaamini kujiunga kwake na Simba kutamsaidia kuinua zaidi kiwango chake kisoka.
Mbiyavanga alisema amepania kuonyesha kiwango chake wakati wa michuano ya Kombe la Kagame na amewataka mashabiki wa Simba wajiandae kupata burudani ya kukata na shoka kutoka kwake na wachezaji wenzake.
Simba imefuzu kucheza fainali ya Kombe la Urafiki baada ya kuichapa Zanzibar All Stars bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa Jumatatu iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara sasa watakutana na Azam katika mechi ya fainali inayotarajiwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam ilitinga hatua hiyo baada ya kuichapa Falcon mabao 2-0.

No comments:

Post a Comment