Wachezaji wa Yanga na Azam wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa CECAFA
Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya mabao yao
Yanga jana iliweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame baada ya kuichapa Azam mabao 2-0 katika mechi kali ya fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Washambuliaji Hamizi Kiiza na Saidi Bahanuzi ndio waliowezesha Yanga kutwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifungia mabao hayo mawili, moja katika kila kipindi.
Katika mechi hiyo iliyohudhuruwa na mashabiki lukuki, Azam ilishindwa kabisa kuonyesha cheche zake kutokana na mfumo uliokuwa ukitumiwa na Yanga wa kujaza mabeki wengi nyuma na kuacha washambuliaji wawili mbele.
Kwa kutumia mfumo huo, washambuliaji wa Azam walishindwa kabisa kuipenya ngome ya Yanga na kucheza zaidi katikati ya uwanja, ambako viungo wake walitawala.
Kilichoiwezesha Yanga kulishambulia lango la Azam mara kwa mara ni wachezaji wake wa kiungo na mawinga wa pembeni kupanda wanafanya mashambulizi na kurudi nyuma wakati lango lao likiwa linashambuliwa.
Kutokana na ushindi huo, Yanga ilizawadiwa kitita cha dola 30,000 za Marekani wakati Azam ilizawadiwa dola 20,000. AS Vita ya DRC ilizawadiwa dola 10,000 kwa kushika nafasi ya tatu baada ya kuichapa APR ya Rwanda mabao 2-1.
No comments:
Post a Comment