KIPIGO ilichokipata Simba kutoka kwa Azam katika mechi ya michuano ya soka ya Kombe la Kagame, leo kilizua tafrani wakati wa kikao cha Bunge mjini hapa.
Tafrani hiyo ilizuka baada ya baadhi ya wabunge kumwandikia ujumbe mwenyekiti wa kikao cha asubuhi, Jenista Mhagama wakimtaka awafikishie ujumbe wenzao wa Simba watumie bidhaa za Azam ili wapate nguvu.
Jenista alisoma ujumbe huo wakati akitoa matangazo baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.
Mara baada ya Jenista kumaliza kusoma ujumbe huo, mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage alisimama na kutaka kujibu, lakini hakupewa nafasi hiyo.
Hata hivyo, majibu ya kebehi hiyo yalitolewa na mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya, ambaye aliwaelezea Yanga kuwa ni wazoefu wa kupigana uwanjani.
Profesa Kapuya alisema Simba haifanani na Yanga, ambao baada ya kufungwa mabao 3-1 na Azam katika mechi ya ligi, waliamua kufanya fujo uwanjani na kuonyesha ufundi wa kupigana kareti.
Simba ilitolewa na Azam katika michuano ya Kombe la Kagame baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Azam. Mechi hiyo ilipigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment