TIMU ya wachezaji nyota wa zamani wa soka duniani, inajiandaa kufanya ziara visiwani Zanzibar kwa ajili ya mchezo maalumu dhidi ya timu ya Zanzibar, ' Zanzibar Heroes'. Mapato yatakayopatikana katika mchezo huo yatatumika kuendeleza mradi wa kuhifadhi mazingira katika eneo litakaloamuliwa na Serikali ya Zanzibar. Uamuzi wa kukileta kikosi hicho cha wachezaji nyota wa zamani wa dunia, wanaounda taasisi ya Global United, umefikiwa na Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Italia, Cesare Prandeli.
Kocha huyo alifikia uamuzi huo baada ya kufanya ziara katika kijiji cha Jambiani kama mtalii na kutoa zawadi ya seti moja ya jezi kwa timu ya kijiji hicho mapema mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar (BTMZ), Khamis Abdallah Said alisema wiki hii mjini hapa kuwa, nyota hao wa dunia watatua Zenji mapema mwakani.
Abdallah alisema tarehe ya ziara na mechi hiyo itatangazwa baada ya kukamilika kwa taratibu mbali mbali muhimu na kwa kutegemea utaratibu utakaoandaliwa na Prandelli.
Taasisi ya Global United, imepanga kujenga shule ya soka visiwani Zanzibar kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza.
Vijana watakaofanya vizuri katika masomo shuleni hapo, watapata nafasi ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
Baadhi ya wanasoka nyota wa zamani wa dunia wanaotarajiwa kuwemo kwenye kikosi hicho ni pamoja na Zinedine Zidane, Luis Figo, Mustafa Hadji, Lucas Radebe, Philemon Masinga, Cafu na wengineo. Ziara ya Prandelli, iliratibiwa na Gerd Winkel, ambaye ni mmiliki wa hoteli ya Zanzibar Spice Island Resort iliyoko Jambiani.
No comments:
Post a Comment