KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 4, 2012

NANCY: SIVUTIWI NA FANI YA UIGIZAJI FILAMU

MREMBO wa zamani wa Tanzania, Nancy Sumari amesema kamwe hajawahi kufikiria kuwa mwigizaji na kwamba hakuna kinachomvutia katika fani hiyo.
Nancy amesema miongoni mwa sababu zinazomfanya asivutiwe na fani hiyo ni kutokuwepo kwa mawazo mapya na vitu vipya katika fani hiyo.
Mwanadada huyo aliyewahi kutwaa taji la mrembo wa Tanzania mwaka 2005, alisema hayo wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Five.
“Kusema kweli sijawahi kufikiria kuwa mwigizaji kwa sababu sidhani iwapo nafiti kuwa mwigizaji. Lakini kikubwa ni kwamba sivutiwi na fani hiyo,”alisema Nancy.
Aliongeza kuwa, tangu fani hiyo ilipoanza kupata umaarufu nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000, haoni ubunifu mpya kutoka kwa wasanii wake.
Mbali na kutokuwepo kwa ubunifu wa vitu vipya, Nancy alisema sura za waigizaji wa tangu wakati huo hadi sasa ni zile zile hali inayosababisha mashabiki wawachoke haraka.
Akizungumzia fani ya urembo nchini, ambayo ilimwezesha kutwaa taji la Afrika mwaka 2005, Nancy alikiri kwamba imeanza kupoteza umaarufu kutokana na kujitokeza kwa kasoro mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya kasoro hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya washindi wa mataji ya kitaifa kukumbwa na kashfa mbalimbali, zinazosababisha fani hiyo ionekane kuwa ya kihuni.
Hata hivyo, Nancy alikanusha madai kuwa fani hiyo ni ya kihuni kwa kusema kuwa, uhuni ni tabia na hulka ya mtu binafsi na kamwe haihusiani na kuwa mrembo.
“Ni kweli fani ya urembo imepoteza hadhi kwa kiasi fulani, si kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,”alisema mwanadada huyo bila kutaka kufafanua vitu vingine kwa undani zaidi.
Nancy havutiwi na ongezeko la watoto wa mitaani, ikiwa ni pamoja na mazingira wanayoishi. Kwa mtazamo wake, maisha wanayoishi watoto hawa ni mabaya na wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa serikali.
“Huwa najisikia vibaya sana kuwaona watoto wa mitaani wanavyorandaranda barabarani. Kuna siku nilipokuwa napita barabarani, mtoto mmoja wa kike alikuja kwenye gari langu na kuniomba pesa.
“Nilipoiangalia hali yake, nilimuonea huruma sana. Ngozi yake ilikuwa imeharibika. Nadhani ni kwa sababu ya kupata lishe duni. Nilipompa pesa, nikamsisitizia kwamba lazima atumie pesa hizo kwenda kula,”alisema.
Nancy ameishauri serikali kujenga vituo maalumu kwa ajili ya watoto wa mitaani ili iwe rahisi kuwasaidia kwa huduma za malazi na chakula kuliko ilivyo sasa, ambapo wanaishi kwa kuomba omba.
Nancy alizaliwa mwaka 1986 mkoani Arusha akiwa mmoja kati ya watoto watano wa Abraham Simango Sumari. Ni ndugu wa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nakaaya Sumari, ambaye aliwahi kushiriki katika shindano la Tusker Project Fame.
Kwa sasa, Nancy ni mmoja kati ya Wakurugenzi wawili wa Kampuni ya Frontline Management Limited. Mkurugenzi mwenzake ni Irene Kiwia.

No comments:

Post a Comment