TIMU ya soka ya Simba mwishoni mwa wiki iliyopita ilicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Express ya Uganda na kutoka nayo suluhu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ilikuwa ya pili kwa Simba kucheza na Express. Zilikutana kwa mara ya kwanza wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, ambapo zilitoka sare ya bao 1-1.
Kabla ya kurudiana na Simba, Express pia ilicheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Yanga kwenye uwanja huo na kukubali kipigo cha mabao 2-1.
Mechi zote mbili zilikuwa na mvuto mkubwa kwa mashabiki wa Simba na Yanga. Mvuto huo ulitokana na ukweli kwamba, kila timu ilipanga kuzitumia kujaribu wachezaji wake wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, wakiwemo kutoka nje ya nchi.
Na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Timu zote mbili zilianika vifaa vyao vipya na kuwafanya mashabiki wawe na hamu kubwa ya kuona uwezo wao na ikiwezekana kuwatambia wapinzani wao.
Kwa upande wa Yanga, iliwachezesha kipa Ally Mustafa Barthez, mabeki Juma Abdul, Kelvin Yondan, Ladslaus Mbogo na washambuliaji Simon Msuva, Frank Domayo, Saidi Bahanuzi na Nizar Khalfan. Wachezaji pekee wa zamani waliocheza mechi hiyo ni Oscar Joshua, Nadir Haroub Cannavaro, Athumani Iddi Chuji, Stephano Mwasika na Hamizi Kiiza.
Nayo Simba iliwachezesha Lino Masombo, Kanu Mbiyavanga, Kigi Makasi, Abdalla Juma na Mussa Mudde, ambao ni wacheaji wapya. Wachezaji pekee wa zamani waliocheza ni Edward Christopher, Shomari Kapombe, Uhuru Selemani na Amir Maftah.
Pamoja na timu zote mbili kuchezesha nyota wao kadhaa wapya, jambo la kufurahisha ni kwamba kila moja iliwatumia wachezaji wengi vijana, ambao walicheza kwa kasi muda wote wa mchezo na kuonyesha soka ya kiwango cha juu.
Katika kikosi cha Yanga walikuwepo wachezaji kama Msuva, Domayo, Juma na Bahanuzi, ambao licha ya kiwango chao kuwavutia mashabiki, wameonyesha kila dalili ya kuwa tegemeo kubwa la klabu hiyo katika miaka miwili ama mitatu ijayo.
Pengine Simba ndiyo iliyowatumia wachezaji wengi zaidi vijana, ambao wamepandishwa kutoka katika kikosi cha pili. Wachezaji hao ni Wilbert Mweta, Hassan Kondo, Abdalla, Edward, Paul Ngelema, Shamte Haruna, Abdalla Seseme, Ibrahim Jeba, Ramadhani Singano na Haroun Athumani.
Kilichofurahisha zaidi ni kwamba Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic alifanya mabadiliko ya wachezaji karibu wanane katika kipindi cha pili, ambapo aliwapumzisha wachezaji wote wazoefu na kuwaingiza chipukizi. Aliwapumzisha Lino, Mbiyavanga, Mudde, Maftah, Uhuru, Kapombe na Christopher.
Pamoja na kufanya mabadiliko hayo makubwa kwa kuwapa nafasi chipukizi wengi, kiwango cha Simba hakikubadilika. Na kwa maoni ya baadhi ya wachambuzi wa soka walioshuhudia mechi hiyo, timu iliyocheza kipindi cha pili ilionyesha kiwango cha juu zaidi kuliko ya kwanza.
Hii ni kwa sababu vijana walioingia kipindi cha pili walikuwa damu changa na kila mmoja alitumia nafasi aliyopewa kuonyesha kiwango chake. Kwa ujumla, wachezaji wote wa Simba waliocheza mechi hiyo walionyesha kiwango cha juu na pengine itakuwa vigumu kwa kocha Milovan kuteua kikosi cha kwanza.
Lengo la safu hii si kuchambua mchezo ulioonyeshwa na Simba na Yanga katika mechi hizo kwa sababu kila shabiki aliyefika uwanjani alishuhudia. Lengo ni kuonyesha umuhimu wa timu za vijana kwa klabu za ligi kuu, ambazo kwa miaka miwili sasa zimekuwa zikiinufaisha Simba kutokana na kuibua vipaji vya chipukizi wengi.
Ni wazi kuwa, uamuzi wa Simba kuwa na timu mbili za vijana kama ilivyo kwa Azam FC unapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa klabu zingine kwa sababu utaziwezesha kuibua vipaji vya vijana wengi na kuwaendeleza badala ya kuendelea kutumia mamilioni ya pesa kusajili wachezaji wapya kutoka klabu zingine ama wa kigeni.
Ni kutokana na kuwa na timu hizo za vijana, ndio sababu klabu ya Simba imekuwa ikitoa wachezaji wengi kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars na timu za vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys na timu ya vijana wa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.
Ushauri wangu kwa viongozi wa klabu zingine za ligi kuu ni kuiga mfano huo wa Simba na Azam, ambazo zimekuwa ziking'ara kila mwaka katika michuano ya Kombe la Uhai, ambayo huzishirikisha timu za vikosi vya pili vya timu zinazoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Nina hakika baada ya miaka michache ijayo, wachezaji chipukizi waliopo kwenye timu za vijana za Simba na Yanga ndio watakaong'ara kwenye vikosi vya Taifa Stars, Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys na hata kuuzwa nje kwa pesa nyingi.
No comments:
Post a Comment