MSANII nyota wa filamu nchini, Vicent Kigosi amesema kamwe hajawahi kumchukia msanii mwenzake, marehemu Steven Kanumba ama kufikiria kumuua kwa sababu yoyote ile.
Vicent, maarufu zaidi kwa jina la Ray amesema, tofauti zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara kati yake na marehemu Kanumba zilikuwa za kawaida na zilitokana na ushindani uliolenga kumpatia kila mmoja wao mafanikio.
Ray alisema hayo Jumatatu iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel 5.
“Mimi na marehemu Kanumba tulikuwa tukiendana kwa vitu vingi sana. Na marafiki kugombana ni vitu vya kawaida, vinaweza kutokea hata kwa ndugu waliozaliwa tumbo moja,”alisema.
“Ugomvi wetu ulikuwa wa kibiashara zaidi, sio wa kuchukiana na kutakiana mabaya. Madai hayo yalikuwa ni uzushi tu. Tulishamalizana kupitia kwa wazazi wetu na siwezi kuwa na roho mbaya kiasi hicho. Tulifitinishwa na watu, ambao tulishawabaini,”aliongeza.
Ray alisema alijisikia vibaya baada ya kusikia uvumi kwamba anahusika na kifo cha Kanumba na kuongeza kuwa ndiyo sababu iliyomfanya aandike waraka mrefu kupitia kwenye blogu yake akikanusha tuhuma hizo.
“Mimi na Kanumba tumetoka mbali sana, from zero to heroes. Mambo yaliyokuwa yakitokea kati yetu ni vitu vidogo sana. Hata kama kungekuwa na tofauti kati yetu, zisingekuwa kama zinavyokuzwa na watu,”alisisitiza.
Kwa mujibu wa Ray, kuna siku alimtania Kanumba baada ya kufika kwenye hafla moja akiwa na gari aina ya Toyota Hiace, lakini baadhi ya watu walimtafsiri vibaya kwa lengo la kuwagombanisha.
Ray alisema hata majina yao ya utani yalilenga ushindani kati yao. Alisema baada ya Kanumba kujitambulisha kwa jina la The Great, aliamua kujiita The Greatest kwa sababu alimchukulia mwenzake kama mdogo wake.
“Kusema ule ukweli, kama kulikuwa na tofauti yoyote kubwa kati yetu, namuomba anisamehe, na mimimi nimemsamehe,”alisema Ray, ambaye hajaoa wala kubahatika kupata mtoto.
Alipoulizwa iwapo alifahamu lolote kuhusu uhusiano wa kimapenzi kati ya Kanumba na Elizabeth Michael ‘Lulu’, msanii huyo alisema hakuwa akifahamu kuhusu jambo hilo.
Alisema hata siku Kanumba alipofariki, alipewa taarifa hizo akiwa kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar es Salaam na alikwenda moja kwa moja kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumzia skendo zinazowakabili mara kwa mara wasanii wa filamu nchini, hasa wa kike, Ray alisema zinatokana na tabia za watu binafsi.
“Unajua, ustaa ni gharama. Baadhi yetu wanapenda sana kuwa na maisha ya juu na matokeo yake wanajiingiza katika mambo ya hovyo,”alisema.
Ray alisema moja ya mipango yake ya baadaye ni kusomea fani hiyo ili aweze kuwa na ujuzi mkubwa zaidi. Alisema kwa sasa anatafuta pesa zitakazomwezesha kupata elimu anayoihitaji.
Kwa mujibu wa Ray, lengo lake lingine ni kuwa na maendeleo makubwa zaidi ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo, ikiwa ni pamoja na kutengeneza filamu zake kwa kiwango cha kimataifa.
Alikiri kuwa, lugha imekuwa tatizo kubwa kwa wasanii wa Tanzania kuweza kupata nafasi ya kucheza filamu za kimataifa. Ametoa mwito kwa wasanii wa fani hiyo kujifunza lugha ya kiingereza kwa gharama yoyote.
Ray alisema hadi sasa ameshatengeneza filamu kati ya 45 na 50, kati ya hizo, 32 zikiwa chini ya kampuni yake ya R & J, ambayo aliianzisha kwa kushirikiana na msanii Blandina Chagula ‘Johari’.
Msanii huyo anavutiwa zaidi na uigizaji wa Jacob Steven ‘JB” na Wema Sepetu. Filamu iliyomsumbua sana kuicheza ni Sista Mary, ambayo bado haijatoka. Ameigiza filamu hiyo kama padri.
Kwa sasa, Ray ana mkataba wa kutengeneza filamu na Kampuni ya Steps. Katika mkataba huo, Ray hutakiwa kutengeneza filamu kati ya tano na sita kwa mwaka kwa gharama zake na kulipwa kulingana na mkataba.
Alisema gharama za kukamilisha filamu zinategemea stori, idadi ya waigizaji na vifaa vinavyotumika kama vile nyumba, magari. Lakini alikiri kuwa, hafahamu lolote kuhusu nakala zinazotolewa na mdhamini wake, ambaye alikiri anaweza kufaidika zaidi.
No comments:
Post a Comment