KLABU ya Coastal Union ya Tanga imemsajili kiungo wa zamani wa klabu ya Yanga, Pius Kisambale.
Habari kutoka ndani ya Coastal Union zimeeleza kuwa, Kisambale ametia saini mkataba wa kuichezea timu hiyo kwa miaka miwili.
Kisambale amejiunga na Coastal Union akitokea Yanga, ambayo aliichezea kwa msimu mmoja uliopita.
Mchezaji huyo ni ndugu wa damu wa kiungo wa klabu ya Yanga, Athumani Iddi, ambaye aliwahi kuzichezea timu za Polisi Dodoma na Simba.
Hata hivyo, haikuwekwa wazi kuhusu malipo ya usajili wa kiungo huyo na kiwango cha malipo ya mshahara atakayokuwa akilipwa kwa mwezi.
Uamuzi wa Coastal Union kumsajili Kisambale umelenga kukiimarisha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mbali na Kisambale, uongozi wa Coastal Union pia unafanya mipango ya kumsajili kiungo wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Coastal Union kimeeleza kuwa, mazungumzo kati ya uongozi na mchezaji huyo wa zamani wa Simba yanakwenda vizuri na anatarajiwa kuwasili mjini Tanga wakati wowote.
No comments:
Post a Comment