MWANAMAMA mkongwe kuliko wote katika muziki wa kizazi kipya, Mwahija Cheka (55) ameibuka na kibao kingine kipya kinachokwenda kwa jina la Good Brother Fella.
Mwahija, maarufu zaidi kwa jina la Bi Cheka, amerekodi wimbo huo kwa kushirikiana na msanii machachari wa muziki wa kizazi kipya, Godzilla.
Mmiliki wa kundi la TMK Wanaume Family, Saidi Fella alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kwa sasa Bi Cheka yupo kwenye maandalizi ya mwisho ya kurekodi wimbo huo.
Fella alisema kwa watakaousikia wimbo huo, watakubaliana na ukweli kwamba, bibi huyo hakupotea njia kujitosa kwenye muziki huo.
Kwa mujibu wa Fella, katika wimbo huo, Bi Cheka amepiga swagga za kutosha na za uhakika kiasi cha kuufanya uonekane kuwa wa aina yake.
Bi Cheka ameutumia wimbo huo kumshuruku Fella, ambaye ndiye aliyemfikisha alipo na kumtoa katika biashara yake ya zamani ya kuuza vitumbua na maandazi.
Mama huyo mkongwe mwenye uwezo wa kuimba aina nyingi za muziki, alianza kutamba baada ya kuibuka na kibao cha Ni wewe, alichomshirikisha Mheshimiwa Temba.
Bi Cheka anaamini kuwa, muziki wa bongo fleva upo kwenye damu yake na moja ya malengo yake ya baadaye ni kufika mbali zaidi.
Kipaji cha mama huyo kilivumbuliwa na Temba, ambaye alikutana naye miaka mitatu iliyopita mjini Morogoro. Tayari Bi Cheka ameshafanya maonyesho kadhaa ya kumtambulisha katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Morogoro.
“Nashukuru nilipokewa vizuri na ninapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wasanii wenzangu wa kituo cha kuendeleza vipaji cha Mkubwa na Wanawe,”alisema mama huyo.
“Kilichonipa moyo zaidi ni kuona kuwa mara baada ya kujaribiwa, wote walisema huyu bibi anajua kuimba, atatufaa, nikapewa nafasi, nikaonyesha vitu vyangu, ”aliongeza.
Pamoja na kuanza kupata umaarufu kimuziki, Bi Cheka alisema maisha yake hayajabadilika na kwamba ataendelea kubaki yule yule na kufanya yote aliyokuwa akiyafanya awali.
No comments:
Post a Comment