KAMATI ya uchaguzi ya klabu ya Yanga imemwengua mgombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti, Ally Mayay kutokana na kuidharau kamati hiyo.
Katibu wa kamati hiyo, Francis Kaswahili alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Mayay ndiye mgombea pekee aliyeenguliwa katika uchaguzi huo baada ya kuwekewa pingamizi.
Kwa mujibu wa Kaswahili, Mayay alitakuwa kuhudhuria kikao cha kusikiliza pingamizi alilowekewa ili kutoa ufafanuzi, lakini alishindwa kufanya hivyo na hakutoa taarifa yoyote.
Uchaguzi mdogo wa Yanga umepangwa kufanyika Julai 15 mwaka huu na usali kwa wagombea unafanyika leo makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Awali, wagombea wanne walikuwa wamewekewa pingamizi, wakiwemo Yussuf Manji na Sarah Ramadhani wanaowania nafasi ya mwenyekiti. Wengine ni Yono Kevella na Clament Sanga wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti.
Hata hivyo,pingamizi hizo zilitupwa baada ya waliokuwa wakiwapinga wagombea hao kushindwa kufika kwenye kikao cha ajili ya kutoa ufafanuzi wa madai yao.
Mbali na Manji na Sarah, wagombea wengine wa nafasi ya mwenyekiti ni John Jambele na Edgar Chibula.
Wagombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti ni Ayoub Nyenzi, Kevela na Sanga.
Wanaowania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ni Lameck Nyambaya, Ramadhani Mzimba, Mohamed Mbaraka, Ramadhani Saidi, Edgar Fongo, Beda Simba, Ahmad Gao na Mussa Katabalo.
Wengine ni George Manyama, Aaron Nyanda, Abdala Bin Kleb, Omary Ndula, Shaaban Katwila, Jumanne Mwammenywa, Abdalla Mbaraka, Peter Haule, Justin Baruti na Abdalla Sharia.
No comments:
Post a Comment