KIPA mpya wa klabu ya Yanga, Ally Mustapha'Barthez' ametangaza vita ya kugombea namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa.
Barthez alijiunga na Yanga hivi karibuni akitokea Simba, akiwa ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Barthez alisema amefurahi kujiunga na Yanga na anaamini kiwango chake kitapanda zaidi kuliko alivyokuwa Simba.
Barthez alisema amejipanga vyema kuhakikisha anajifua kwa nguvu zote ili amshawishi kocha ampe namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.
Alisema anawashukuru viongozi wa kamati ya usajili ya Yanga kwa kumpatia nafasi hiyo na kusisitiza kuwa, kamwe hawezi kuwaangusha.
"Ninaushukuru uongozi wa Simba kwa kunilea vizuri katika kipindi chote nilipokuwa nikiichezea timu hiyo na kama kuna niliowahi kuwakera, naomba wanisamehe, ‘ alisema.
Kipa huyo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa kipa namba moja wa timu hiyo, Yaw Berko kutoka Ghana na kipa namba mbili, Saidi Mohamed.
Akizungumzia ujio wa Barthez, Kocha wa makipa wa Yanga, Mfaume Athumani alisema anaamini utaongeza ushindani kwa makipa wengine wa timu hiyo.
Mfaume alisema Barthez ni kipa mzuri na mwenye uzoefu wa michuano ya ligi na kimataifa kutokana na kuichezea Simba kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment