MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Kisutu Dar es Salaam jana ilishindwa kuendelea kusikiliza kesi ya tuhuma za mauaji inayomkabili msanii nyota wa filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' kutokana na kutokuwepo kwa jalada halisi la kesi yake.
Lulu (17) alifikishwa katika mahakama hiyo kama kawaida, lakini hakupandishwa kizimbani kutokana na jalada la kesi hiyo kupelekwa Mahakama Kuu.
Msanii huyo aliwakilishwa mahakamani hapo na wakili wake, Peter Kibatala anayemtetea.
Wakili wa serikali, Keneth Sekwao alidai kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika, ambapo aliomba ipangwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Kufuatia ombi hilo, Hakimu Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo, alisema itatajwa tena Julai 2 mwaka huu.
Lulu alifikishwa mahakama hapo saa tatu asubuhi akiwa katika gari la magereza. Ilipofika saa nne, Lulu aliondolewa mahakamani hapo akiwa katika gari la magereza na kuwaacha hoi waandishi wa habari waliokuwa wakimsubiri ili waweze kumpiga picha.
Habari za kuaminika zilizopatikana mahakamani hapo zilidai kuwa, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kutoa uamuzi wa kuchunguza umri wa Lulu, kila kitu kilisimamishwa kwa vile jalada halisi halipo.
Kwa mujibu wa habari hizo, kabla ya uamuzi wa Mahakama Kuu kutolewa, kesi hiyo ilipangazwa kutajwa jana na kwamba kwa kawaida, baada ya uamuzi huo, Jaji anayesikiliza maombi ya uchunguzi wa umri wa msanii huyo alipaswa kumwandikia barua Hakimu Augustina ili kumweleza kuhusu kusimamishwa kwa kesi hiyo mahakamani hapo.
Habari hizo ziliendelea kudai kuwa, hakimu anayesikiliza kesi hiyo alipaswa kupewa nakala ya uamuzi huo na kwamba mshitakiwa hakupaswa kufikishwa mahakamani hadi uamuzi kuhusu utata wa umri utakapotolewa.
Jaji Fauz Twaib wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam anatarajia kutoa uamuzi kuhusu utata huo wa umri Juni 25 mwaka huu.
Awali, Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu ilikataa ombi la upande wa utetezi la kutaka ufanywe uchunguzi kuhusu umri sahihi wa Lulu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Lulu anadaiwa kuwa Aprili 7 mwaka huu, eneo la Sinza Vatican, Dar es Salaam, alimuua msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Marehemu Kanumba alizikwa Aprili 10, mwaka huu kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam katika mazishi, ambayo yalihudhuriwa na maelfu ya watu, wakiwemo viongozi wa serikali.
No comments:
Post a Comment