KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 18, 2011

JABIR AZIZ: Mawazo yangu ni Ughaibuni tu



MMOJA wa wanasoka waliojipatia umaarufu mkubwa nchini kutokana na umahiri wake wa kusakata kabumbu ni mshambuliaji Jabir Aziz wa Azam FC. Kabla ya kujiunga na Azam, Jabir alikuwa akichezea Simba, lakini hakuweza kupata mafanikio makubwa. Makala hii ya Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE inaelezea safari ya Jabir kisoka na matarajio yake ya baadaye.



SWALI: Ulipokuwa ukichezea Simba, haukupata mafanikio makubwa kisoka kama ilivyo hivi sasa kwa Azam FC. Unaweza kueleza nini siri kubwa ya mafanikio yako?
JIBU: Kwa kweli sina jipya zaidi ya kujituma na kuhakikisha ninakuwa fiti ili niweze kumshawishi kocha kunipanga katika michezo zijazo.
Pamoja na hayo, huwa najisikia furaha kuona mchezaji mwenzangu wa Tanzania anapata maendeleo na hiyo inakuwa changamoto kwangu kuhakikisha najifua ili nami niweze kumfikia ama kumzidi.
SWALI: Nimesikia kupitia viongozi wako wa Azam kwamba umepata ofa ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa nchini Norway je, taarifa hizo ni za kweli?
JIBU: Ni kweli nimepata ofa hiyo, lakini viongozi wangu ndio wanaofahamu zaidi kwani kila kitu nimewaachia wao washughulikie.
Licha ya ofa hiyo, binafsi nimekuwa nawasiliana na baadhi ya mawakala wa soka ili waweze kunitafutia timu nje ya nchi. Lengo langu ni kuongeza kipato changu na pia kutumia ujuzi, ambao nitapata huko nje ya nchi kutoka kwa makocha ili niweze kuja kuinufaisha nchi yangu ya Tanzania.
Vilevile napenda nikiwa nje ya nchi, niitumie nafasi hiyo kuitangaza nchi yangu kwa kuvaa vitu mbalimbali, vikiwemo vinavyotangaza utalii wa Tanzania.
SWALI: Tukirudi nyuma, unazungumziaje kuhusu ushiriki wa Azam FC katika michuano ya ligi kuu msimu uliopita?
JIBU: Kufanya vibaya kwa Azam katika michuano ya ligi kuu ya msimu uliopita kumetupotezea malengo yetu mengi. Moja ya malengo hayo, tuliyokuwa tumejiwekea ni kutwaa ubingwa.
Zipo sababu nyingi zilizotufanya tushindwe kutwaa ubingwa. Miongoni mwa sababu hizo ni kikosi chetu kuwa na wachezaji wengi wapya, hivyo hakikuwa kimejiandaa vyema. Hali hiyo ilichangia kutufanya tupoteze mechi nyingi.
Nina hakika kasoro hiyo na nyinginezo hazitajitokeza tena msimu ujao. Nina hakika kikosi chetu kitakuwa moto wa kuotea mbali.
Nasema hivyo kwa sababu nimegundua kuwa, wachezaji wengi wanaosajiliwa na Azam wana vipaji vya hali ya juu vya kusakata kabumbu na kuipa matokeo mazuri. Kinachohitajika ni sisi wachezaji kuonyesha moyo wa kizalendo na kulipa fadhila kwa wamiliki wa klabu.
SWALI: Nini ushauri wako kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili michuano ya ligi kuu iwe ya kiwango cha hali ya juu?
JIBU: Binafsi nina mambo mawili makubwa ya msingi. La kwanza ni kuwaomba waamuzi wanaopangwa kuchezesha mechi za michuano hiyo, kuzingatia sheria zote 17 za soka badala ya kuchezesha kwa upendeleo.
Nimefanya uchunguzi wangu kwa muda mrefu na kugundua kwamba, baadhi ya waamuzi wanashindwa kuzitafsiri vyema sheria za soka na kutoa maamuzi, ambayo kidogo yanatatanisha.
Jambo la pili, nawaomba viongozi wa TFF na wale wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom, ambao ndio wadhamini wakuu wa ligi hiyo, kuangalia suala la bima ya wachezaji.
Hili ni jambo la muhimu sana kutokana na wachezaji wengi kuumia na kukosa haki zao za msingi na wengine kupata ulemavu, hasa wale ambao wanachezea timu, ambazo hazina wadhamini.
Ni vyema TFF na Vodacom walitazame jambo hilo kwa umakini na ikiwezekana, iwapo wataongeza mkataba wa udhamini wa ligi hiyo miaka ijayo, suala hilo lipewe kipaumbele.
Napenda suala la bima lipewe nafasi katika mkataba mpya kati ya Vodacom na TFF ili wachezaji, ambao wanachezea timu zisizokuwa na wadhamini, waweze kupata malipo yao kila wanapoumia katika mechi za ligi badala ya kutelekezwa.

No comments:

Post a Comment