'
Thursday, May 5, 2011
Rage awaonya wenye risiti za Simba
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amewataka wanachama au mtu yeyote mwenye risiti za klabu hiyo kuziwasilisha kwa uongozi mara moja.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Rage alisema amebaini kuwa, wapo baadhi ya viongozi wanaomiliki risiti za klabu hiyo kinyume cha sheria.
Rage alisema, kufuatia kubainika kwa jambo hilo, wanachama wa Simba wanapaswa kuwa makini, hasa wakati wa kulipia ada zao za uanachama.
"Nimegundua wapo baadhi ya watu wanazo risiti za klabu, hivyo ni vyema wakazirudisha klabuni mara moja ili wapewe viongozi wa sasa na ninawaomba wanachama walipie ada zao benki si kwa mtu binafsi,"alisema.
Mwenyekiti huyo alisema, kwa mujibu wa utaratibu mpya uliobuniwa na uongozi wa sasa, hairuhusiwi kwa pesa za klabu kutolewa benki bila idhini ya wanachama.
Rage alisema katika kipindi hiki cha uongozi wake, wataendelea kuweka wazi kila kitu kinachoihusu Simba ili wanachama waweze kuelewa kinachoingia na kutoka klabuni.
"Hatutaki kuweka maswali katika suala la mapato na matumizi ya klabu yetu, kila kitu kitafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa,hakuna jingine,"alisema kiongozi huyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment