BAADHI ya mashabiki wa muziki wa taarab wa Jiji la Dar es Salaam, wamemlalamikia kiongozi wa kundi la Jahazi, Mzee Yusuph kwa madai kuwa amezidisha maringo wakati wa maonyesho ya kundi lake.
Wakizungumza na Burudani kwa nyakati tofauti kwenye kumbi mbalimbali za starehe, mashabiki hao wamedai kuwa, Mzee amekuwa na tabia ya kuchelewa kufika ukumbini.
Mbali na kuchelewa kufika ukumbini, mashabiki hao wamedai kuwa, kiongozi huyo wa kundi la Jahazi amekuwa na kawaida ya kuimba nyimbo chache anapofika ukumbini na kisha kutoweka.
Katika onyesho moja la kundi hilo, lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam, mwandishi wa habari hizi alimshuhudia kiongozi huyo wa Jahazi akifika ukumbini saa saba usiku wakati wenzake wakiwa wameshaanza onyesho.
Licha ya kufika ukumbini akiwa amechelewa, Mzee aliimba nyimbo tatu na baadaye kutoweka, hali iliyolalamikiwa na mashabiki wengi waliodai kuwa, kiongozi huyo wa Jahazi ameanza kuwa na maringo.
“Hii haikuwa tabia ya kawaida kwa Mzee Yusuph. Siku hizi amebadili mno, sijui anachoringia ni kitu gani,” alilalamika shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Rehema Hassan, mkazi wa Magomeni.
Shabiki mwingine anayefahamika kwa jina la Hussein Makoroboi alisema, kwa staili hiyo, kundi la Jahazi litaanza kupoteza mashabiki kutokana na wasanii wake kuzidisha maringo.
Hivi karibuni, kundi hilo liliwasimamisha waimbaji wake wawili nyota, Leila Rashid na Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ kwa tuhuma za makosa ya utovu wa nidhamu.
Waimbaji hao walisimamishwa kwa madai ya kuchelewa kufika kwenye maonyesho, kujiona wao bora kuliko wenzao na pia kutohudhuria mazoezini mara kwa mara.
Juhudi za kumpata Mzee ili ajibu malalamiko ya mashabiki hao hazikuweza kufanikiwa kwa vile simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.
No comments:
Post a Comment