MIAMBA ya soka barani Ulaya, Manchester United ya England na Barcelona ya Hispania, inashuka dimbani keshokutwa katika mechi ya fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Mechi hiyo, itakayopigwa kwenye uwanja wa Wembley mjini London nchini Uingereza, inatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa vile kila timu imepania kushinda ili kutwaa ubingwa.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu kwa Manchester na Barcelona kukutana katika fainali ya michuano hiyo. Zilikutana kwa mara ya mwisho mwaka 2009 mjini Rome, Italia ambapo Barcelona iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Barcelona na Manchester United zimewahi kukutana katika michuano hiyo mara 11, ambapo kila moja imeshinda mechi tatu. Timu hizo pia zimetwaa ubingwa wa Ulaya mara tatu kila moja.
Timu zote mbili zinashuka dimbani huku kila moja ikiwa imetwaa ubingwa wa ligi ya nchi yake. Manchester United imetwaa ubingwa wa ligi hiyo mara nne katika kipindi cha miaka mitano wakati Barcelona imetwaa ubingwa mara tano katika kipindi cha miaka saba.
Pamoja na timu zote kuundwa na wachezaji wengi nyota, macho ya mashabiki wengi wa soka duniani yanatarajiwa kuwa kwa wachezaji wawili, Wayne Rooney wa Manchester United na Lionel Messi wa Barcelona.
MESSI
Akizungumzia mechi hiyo hivi karibuni, Messi alisema ushindi wa taji hilo dhidi ya Manchester United ni muhimu kwake kuliko kufunga bao ndani ya ardhi ya Uingereza.
Messi alisema hawapaswi kuidharau Manchester United kwa kigezo cha kuifunga katika mechi yao ya mwisho mwaka juzi na kwamba ushindi keshokutwa ni muhimu kwake kuliko kuibuka mfungaji bora.
Katika msimu huu, Messi ameifungia Barcelona mabao 52, mabao 11 akiyafunga katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya. Anaweza kuweka rekodi ya kufunga mabao 12, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Ruud van Nistelrooy.
Messi alisema kwake, anaweka mbele zaidi ushindi wa Barcelona katika michuano hiyo kuliko rekodi yake binafsi. “Mabao yanakuwa muhimu pale tu mnaposhinda mechi,” alisema.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina anaamini kuwa, kikosi cha Manchester United, kinachofundishwa na Kocha Sir Alex Ferguson, kitakuwa tishio na amewaonya wachezaji wenzake wasiwadharau wapinzani wao.
“Nawaheshimu sana, ni timu nzuri na wanaye kocha mwenye rekodi nzuri na wachezaji wake ni tishio. Kukaa kwenye klabu miaka mingi na kushinda mataji mengi ni heshima kubwa,”alisema.
Messi alizaliwa Juni 24, 1987 katika mji wa Rosario nchini Argentina. Ni mchezaji anayevaa jezi namba 10 katika klabu yake ya Barcelona, aliyojiunga nayo mwaka 2005, akitokea kikosi cha pili cha klabu hiyo.
Aliitwa kwenye timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 20 ya Argentina mwaka 2005 na baadaye timu ya vijana wa chini ya miaka 23. Aliichezea timu ya taifa ya wakubwa kwa mara ya kwanza mwaka 2005. Ameichezea timu hiyo mechi 55.
ROONEY
Rooney alitoa mpya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kushangilia ushindi wa Manchester United katika ligi kuu ya England kwa kuchora namba 19 kifuani kwake.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Everton, alionyesha mchoro huo mara baada ya Manchester United kutoka sare ya bao 1-1 na Blackburn Rovers na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya 19.
Rooney ndiye aliyeifungia Manchester United bao hilo la pekee. Mara baada ya mchezo huo, aliituma picha aliyopiga kwenye vyumba vya wachezaji, ikionyesha mchoro huo, kwenye mtandao wa Twitter. Hiyo ilikuwa zawadi aliyowapa mashabiki wa klabu hiyo.
Ushindi wa Manchester United uliiwezesha kuipiku rekodi ya Liverpool, iliyotwaa ubingwa wa England mara 18.
“Hakuna aliyetarajia Rooney angeituma picha hiyo kwenye mtandao wa Twitter. Alikuwa kama kichaa kuliko tulivyofikiri,”alisema mshambuliaji mwenzake, Michael Owen.
Rooney anaamini kuwa, zawadi pekee iliyobaki kwa mashabiki wa Manchester United ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ulaya kwa mara ya nne.
Mshambuliaji huyo ghali nchini England kwa sasa, alizaliwa Oktoba 24, 1985. Alicheza michuano ya fainali za Ulaya kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na kufunga mabao manne.
Aliitwa kwenye kikosi cha England kwa mara ya kwanza mwaka 2003. Aliichezea timu hiyo katika fainali mbili za Kombe la Dunia mwaka 2006 na 2010.
Alishinda tuzo ya mwanasoka bora wa England mara mbili mwaka 2008 na 2009. Hadi ilipofika Machi mwaka huu, aliweka rekodi ya kucheza mechi 79 za kimataifa na kufunga mabao 26.
Rooney alijiunga na Manchester United msimu wa 2004-05, akiwa na umri wa miaka 18, akitokea Everton. Usajili wake uliigharimu Manchester United kitita cha pauni milioni 25.6 za Uingereza.
Mara baada ya kujiunga na Manchester United, alikabidhiwa jezi namba nane, lakini baadaye alipewa jezi namba 10, iliyokuwa ikitumiwa na Ruud van Nistelrooy.
No comments:
Post a Comment