'
Wednesday, May 18, 2011
Aki na Ukwa wawekwa kikaangoni
LAGOS, Nigeria
BAADHI ya wazazi nchini Nigeria wametishia kuzipiga marufuku filamu zilizochezwa na waigizaji machachari, Aki na Ukwa kwa madai kuwa, zinatoa mafundisho mabaya kwa watoto wao.
Wazazi hao wamesema, filamu nyingi zinazochezwa na vijana hao wenye vimo vifupi, zinaonyesha dharau kwa watu wazima na kuwafundisha wizi vijana. “Vijana wengi wamekuwa wakiiga matukio yanayofanywa na Aki na Ukwa kwenye filamu wanazocheza, hivyo kuathirika,” amesema mmoja wa wazazi hao, aliyehojiwa na mtandao wa Nigeriafilms.
Mzazi mwingine alisema, matukio ya wizi yamekuwa yakiongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma, wahusika wakuu wakiwa vijana wa umri mdogo kutokana na kuiga tabia za wacheza filamu hao.
Wazazi hao wamedai kuwa, vijana wengi wa umri mdogo nchini Nigeria wanapenda kuishi maisha yanayofanana na yale ya Aki na Ukwa bila kujua kuwa ni ya uigizaji.
Baadhi ya wazazi wamehoji ni kwa nini filamu zote wanazoshiriki kucheza vijana hao, zinaonyesha vitendo vya uovu katika jamii badala ya mafundisho mema.
“Kama huonyeshi matendo mazuri kwa vijana wako nyumbani, lazima watakuiga,”alisema mmoja wa wazazi hao.
Mzazi huyo alisema wanawapa changamoto waandaaji wa filamu wa Nollywood, kubadili mwelekeo kwa kuandaa sinema, ambazo haziwezi kuathiri maisha ya vijana wao.
“Wanapaswa kutengeneza filamu zenye mwelekeo chanya. Vijana ni wepesi wa kuiga na wakifanya hivyo, wanaonyesha picha mbaya ya Wanigeria,”aliongeza.
Aki na Ukwa ni miongoni mwa wacheza filamu waliojipatia sifa na umaarufu nchini Nigeria kutokana na kucheza filamu nyingi na zinazopendwa na vijana wengi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment