BAADHI ya mashabiki wa soka nchini wameweka nadhiri, viapo na wengine kucheza kamari ya fedha kuhusu mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Mchezo huo utakaopigwa keshokutwa kwenye uwanja wa Wimbley mjini London, England umewagawa mashabiki wa soka nchini, kila upande ukiitabiria mema timu unayoipenda.
Kwa kipindi cha takriban wiki mbili sasa, waandishi wa habari wa gazeti hili, wameshuhudia tambo na mabishano kutoka kwa mashabiki wa klabu hizo mbili kwenye kumbi mbalimbali za buudani za mjini Dar es Salaam.
Kwenye hoteli ya New Happy iliyopo eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, shabiki Hamad Jella, ameitabiria Barcelona ushindi huku akisema, iwapo timu hiyo itashindwa kuchukua ubingwa, ataacha kunywa pombe maisha yake yote na itakuwa mara ya mwisho kwenda hapo.
“Barcelona ikishindwa kutwaa ubungwa, naacha kunywa pombe na itakuwa mara yangu ya mwisho kuja kwenye baa hii,” alisikika shabiki huyo akiweka nadhiri.
Kwa upande wake, Frank Kamugisha maarufu kwa jina la Frank Manchester alisema, ameanza kushangilia ubingwa kwa kuwa dalili zote zinaonyesha Man U itashinda.
“Hii siyo mara ya kwanza kukutana na Barcelona kwenye fainali, mara ya mwisho walitufunga na baada ya hapo tumewafuatilia na kujua udhaifu wao, lazima tutashinda,” alisema Frank.
Katika klabu ya Italian House eneo la Tabata Mawenzi, mashabiki wa timu zote wameanza kutambiana huku kila upande ukipanga kufunga bendera kubwa za timu zao nje ya klabu hiyo.
“Nipo tayari kuweka shilingi laki moja kama Manchester itafungwa,” alisikika akisema Joseph Michael, ambaye alipingwa na shabiki wa Barcelona, anayefanya kazi ya uwakili, lakini hakutaka jina lake litajwe.
Mashabiki hao kila mmoja ameweka shilingi laki moja, akifagilia timu yake kuibuka na ushindi. Hata hivyo, dakika tisini ndizo zitakazomua fedha hizo zitakwenda kwa nani.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa baadhi ya maeneo nchini, mfalme wa soka duniani Pele na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa England, Garry Lineker wameitabiria ushindi Manchester United.
Kwa upande wake, Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amekiri kuwa Barcelona ya mwaka huu ni nzuri kuliko ilivyokuwa mwaka 2009.
No comments:
Post a Comment