Ochan auzwa TP Mazembe kwa mil 150/-
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ameionya Yanga kuwa, inafanya makosa makubwa kutaka kumsajili tena mshambuliaji Kenneth Asamoah bila kufanya mazungumzo na klabu yake ya FK Jagodina ya Serbia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Rage alisema kwa mujibu wa kanuni za usajili, viongozi wa klabu hawapaswi kuzungumza na mchezaji kabla ya kupata ruhusa ya viongozi wake.
Rage alikiri kuwa, ni kweli kwamba Yanga imeshafanya mazungumzo na mchezaji huyo kwa ajili ya kumsajili tena msimu ujao na anatarajiwa kutua nchi leo, lakini wanaweza kukwama kwa vile hawajapata ridhaa ya klabu yake.
“Kanuni zinasema wazi kwamba, klabu ndizo zinazopaswa kufanya mazungumzo kwanza kuhusu usajili wa mchezaji ndipo baadaye yanafuata mazungumzo ya mchezaji na klabu inayotaka kumsajili,”alisema Rage.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, wao bado wanaendelea kufanya mipango ya kumsajili mshambuliaji huyo, lakini wameamua kwanza kuzungumza na klabu yake.
“Kama tutakubaliana na viongozi wa klabu yake, nina hakika tunaweza kumsajili mshambuliaji huyo,”alisema.
Hivi karibuni, Rage alikaririwa akisema kuwa, wamemtuma Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kwenda Serbia kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wa klabu hiyo baada ya Asamoah kuwasilisha maombi ya kutaka asajiliwe na klabu hiyo.
Asamoah, ambaye alikuwa akicheza soka ya kulipwa nchini Serbia, alisajiliwa na Yanga msimu uliopita, lakini alishindwa kuichezea baada ya klabu hiyo kushindwa kumlipia ada ya uhamisho.
Usajili wa Asamoah uligubikwa na utata mkubwa msimu uliopita baada ya klabu yake ya FK Jagodina ya Serbia kugoma kumpatia uhamisho wa kimataifa (ITC) baada ya Yanga kushindwa kumlipia ada ya uhamisho.
Katika hatua nyingine, klabu ya Simba imesema imemuuza kiungo wake, Patrick Ochan kutoka Uganda kwa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa gharama ya sh. milioni 150.
Rage alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uongozi wa TP Mazembe umekubali kutoa kiasi hicho cha fedha baada ya kuridhishwa na kiwango cha Ochan.
Ochan anakuwa mchezaji wa pili wa Simba kuuzwa kwa TP Mazembe katika kipindi cha mwezi mmoja. Hivi karibuni, Simba pia ilimuuza mshambuliaji wake, Mbwana Samatta kwa kiasi hicho cha pesa kwa TP Mazembe.
Mabingwa hao wa Afrika walivutiwa na Samatta na Ochan wakati timu hiyo ilipokutana na Simba katika mechi za raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika zilizochezwa Machi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment