KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 18, 2011

Mwaikimba apigwa 'stop'


UONGOZI wa timu ya soka ya Kagera Sugar umesema hauna taarifa yoyote kuhusu mshambuliaji wao, Gaudence Mwaikimba kutakiwa na timu ya Moro United.
Mbali na kutokuwa na taarifa hiyo, uongozi wa Kagera Sugar umesema haupo tayari kumuuza mshambuliaji huyo kwa vile bado wanamuhitaji katika msimu ujao wa ligi.
Kauli na msimamo huo ulitolewa juzi na mratibu wa timu hiyo, Mohamed Hussein alipozungumza na gazeti la Burudani kutoka mjini Bukoba.
Hussein alisema wamekuwa wakisikia taarifa za mchezaji huyo kusajiliwa na Moro United kupitia kwenye vyombo vya habari, lakini hawajawahi kufanya mazungumzo yoyote na uongozi wa timu hiyo.
"Mimi ninachojua ni kwamba, Mwaikimba ni mchezaji wa Kagera Sugar na bado tuna mkataba naye, hao Moro United hawajawahi kufika kwetu kwa ajili ya mazungumzo ya kumtaka mchezaji huyo,"alisisitiza mratibu huyo.
Akizungumzia maendeleo ya usajili wa timu yake kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, Hussein alisema bado wanaendelea kuziba mapengo ya wachezaji walioachwa na waliouzwa.
Alisema lengo la timu yake ni kusajili wachezaji wengi wazalendo na kuongeza kuwa, wamepanga kufanya hivyo kupitia michuano ya Kombe la Taifa.
Mbali na kusajili wazalendo, Hussein alisema pia kuwa, wamefanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji kutoka nchi za Kenya, Uganda na Burundi kwa ajili ya usajili huo.

No comments:

Post a Comment