KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 18, 2011

Hii ndiyo Wydad Casablanca, itakayocheza na Simba


WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika, Simba mwishoni mwa wiki iliyopita walishinda rufani yao dhidi ya mabingwa watetezi, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Katika rufani hiyo, iliyowasilishwa mwezi uliopita kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Simba iliilalamikia TP Mazembe kwa kumchezesha mchezaji Janvier Besala Bokungu katika mechi ya awali kati yao kinyume cha kanuni za usajili.
Simba ilidai kuwa, Bokungu hakuwa mchezaji halali wa TP Mazembe kwa vile bado alikuwa na mkataba na klabu yake ya zamani ya Esperance ya Tunisia. Simba ilitolewa katika michuano hiyo na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 6-3.
Kufuatia rufani hiyo, CAF imeiondoa TP Mazembe katika michuano hiyo na kuipatia nafasi hiyo Simba, ambayo sasa imepangwa kucheza mechi moja na Wydad Casablanca ya Morocco kati ya Mei 27 hadi 29 katika uwanja huru utakaotangazwa baadaye.
Mshindi wa mechi hiyo, atacheza hatua ya makundi ya ligi hiyo katika kundi B. Timu zingine zilizopangwa kundi hilo ni Al Ahly ya Misri, EST ya Tunisia na Moloudia Club ya Algeria.
Iwapo Simba itapoteza mechi hiyo, itaangukia katika michuano ya Kombe la Shirikisho na kucheza hatua ya mtoano dhidi ya DC Motema Pembe ya Congo.
Kurejeshwa kwa Simba katika michuano hiyo kumezua maswali mengi. Wapo wanaoipongeza Simba kwa kuweza kutetea haki yake na wengine wanaionea huruma kwa vile kwa sasa haina kikosi kinachoweza kuhimili mikikimikiki ya Wamorocco hao.
Tangu kumalizika kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, wachezaji wengi wa Simba walitawanyika. Wapo waliouzwa kwa klabu zingine za nje kama vile Mbwana Samatta na Patrick Ochan na wapo waliouzwa kwa mkopo kwa klabu zingine.
Tayari pia Simba ilishatangaza kuwatema wachezaji wengine kadhaa kwa madai ya viwango vyao kushuka na wengine walishutumiwa kwa kuwashawishi wenzao wacheze chini ya kiwango ili timu hiyo ishindwe kutetea ubingwa wake. Simba ilimaliza ligi hiyo ikiwa ya pili.
Hata hivyo, inatia moyo kuona kwamba Simba imeshaanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya pambano hilo na wachezaji wake kadhaa wa zamani wameshaanza kuripoti kambini isipokuwa Emmanuel Okwi aliyeko Afrika Kusini, Hillary Echessa aliyemaliza mkataba wake na Joseph Owino aliyejiunga na Azam. Timu hiyo ipo chini ya Kocha Moses Basena kutoka Uganda.
Wachezaji wa Simba walioripoti kwenye mazoezi ya timu hiyo hadi juzi ni Uhuru Selemani, Rashid Gumbo, Kelvin Yondani, Amri Kiemba, Juma Nyoso, Shija Mkina, Juma Jabu, Patrick Ochan, Nico Nyagawa, Jerry Santo, Abdulrahim Humud, Salum Gila, Mohamed Banka, Salum Aziz na Juma Kaseja.
Swali kubwa wanalojiuliza mashabiki wa soka nchini ni iwapo Simba itaweza kuimudu Wydad Casablanca bila kuwa na mazoezi ya muda mrefu. Wapinzani wao hao bado wanashiriki katika michuano ya ligi ya Morocco.
Wydad ni timu yenye mafanikio makubwa nchini Morocco, ikiwa imetwaa ubingwa wa nchi hiyo mara 12, sawa na FAR Rabat. Wydad pia imeshika nafasi ya pili mara tisa wakati FAR wameshika nafasi hiyo mara sita.
Raja Casablanca, ambayo ni maarufu zaidi nchini kutokana na kupambana na Yanga mwaka 1998, ni ya tatu kwa kuchukua ubingwa wa Morocco mara sita.
Wydad pia imeweka rekodi ya kushinda Kombe la Morocco mara tisa wakati FAR Rabat imelinyakua mara 11. Raja Casablanca ni ya tatu kwa kulitwaa mara sita.
Katika historia yake, Wydad imetwaa ubingwa wa Afrika mara moja mwaka 1992. Mwaka 2002 walitwaa Kombe la Washindi la Afrika na mwaka 1994 walitwaa ubingwa wa nchi za Afrika zenye asili ya kiarabu.
Kikosi cha Wydad kimesheheni nyota wengi wanaocheza katika ligi hiyo na kutoka nje ya nchi. Mmoja wa washambuliaji hao nyota kutoka nje ni Luiz Jeferson Escher kutoka Brazil, ambaye alinunuliwa msimu huu kutoka Kawkab Marrakech ya huko huko Morocco.
Nyota wengine, ambao timu hiyo inajivunia ni pamoja na jean Louis Paschal Angan na Fabrice N’Guessi, ambaye ni raia kutoka Congo. Angan ni mchezaji wa kimataifa wa Benin.
Katika wachezaji wa nyumbani, Wydad inajivunia nyota wake, Youness Mankari. Kocha Mkuu wa timu hiyo ni Fakhreddine Rahji.

No comments:

Post a Comment