KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 26, 2011

Muumini bado aikumbuka Bwagamoyo Sound


MTUNZI na mwimbaji nyota wa muziki wa dansi nchini, Mwinjuma Muumini amesema yupo katika hatua za mwisho za maandalizi ya albamu ya bendi yake ya zamani ya Bwagamoyo Sound.
Muumin aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa juzi kuwa, amebakiza nyimbo mbili kabla ya kukamilisha albamu hiyo, itakayokuwa na nyimbo sita.
Mwimbaji huyo wa zamani wa bendi za Mchinga Sound na African Revolution alisema, albamu yake hiyo itajulikana kwa jina la ‘Nafsi haina urithi’.
Alivitaja vibao vingine vitakavyokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Mwanamtiti Malunde’, ‘Cute Baby’, ‘Natafuta mume’, ‘Ufukara Jeraha’, ‘Udugu wa mashaka’.
Mwinjuma alisema amerekodi albamu hiyo kwa kuwashirikisha wanamuziki wa zamani wa bendi hiyo na kwamba hatarajii kufanya uzinduzi.
“Nitaiingiza albamu hii moja kwa moja sokoni, sitafanya uzinduzi kama ilivyo kwa bendi zingine,”alisema mwimbaji huyo, ambaye kwa sasa yupo bendi ya Twanga Pepeta International.
Aliwataja baadhi ya wanamuziki alioshirikiana nao kurekodi albamu hiyo kuwa ni Geoge Gama, Yahya Mkango, Venas Joseph, Wera Baba, Karama Legesu na marehemu Mwamvita Ramadhani.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake wa kuivunja Bwagamoyo Sound na kujiunga na Twanga Pepeta, mwanamuziki huyo alisema, umetokana na kutafuta maslahi zaidi.
Alikiri kuwa, bendi yake hiyo ilishindwa kukamata soko la muziki nchini kutokana na kuwepo kwa bendi nyingi na kusisitiza kuwa, kwa sasa ameamua kuweka maskani ya kudumu Twanga Pepeta.
Kwa mujibu wa Mwinjuma, tayari ameshatunga kibao kimoja kinachokwenda kwa jina la ‘Penzi la shemeji’, ambacho kitakuwa cha kumi na moja kwenye albamu mpya ya bendi hiyo.
Alisema anachokifanya kwa sasa ni kusoma muziki wa bendi hiyo na kujipanga upya kwa sababu imepita miaka mingi tangu alipokuwa akipigia bendi ya African Revolution.
“Nimepania kurudisha heshima yangu kimuziki, iliyopotea baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu bila kusikika kwa mashabiki,”alisema.
Ameushukuru uongozi wa bendi hiyo pamoja na wanamuziki wenzake kwa kumpa mapokezi mazuri na kuongeza kuwa, atahakikisha anatimiza malengo waliyojiwekea.

No comments:

Post a Comment