KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 18, 2011

Asamoah aitesa Yanga



Ataka alipwe mil 19.5/-

Niyonzima amwaga wino

Yamtosa ‘pro’ kutoka Uganda


KAMATI ya Usajili ya klabu ya Yanga, inahaha kusaka dola 13,000 za Marekani (sh. milioni 19.5) kwa ajili ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seif Ahmed alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Asamoah anataka alipwe kiasi hicho cha fedha ili akaziwasilishe kwa klabu yake ya zamani ya FK Jagodina ya Serbia.
Kwa mujibu wa Seif, FK Jagodina inataka ilipwe fedha hizo ili iweze kutoa uhamisho wa kimataifa wa mshambuliaji huyo, aliyejiunga na Yanga tangu mwaka jana.
Asamoah alisajiliwa na Yanga msimu uliopita, lakini alishindwa kuichezea katika michuano ya ligi na ya kimataifa, kufuatia timu hiyo kushindwa kufikia makubaliano na FK Jagodina kuhusu malipo ya uhamisho wake.
Mshambuliaji huyo aliwasili nchini mwishoni mwa wiki iliyopita na kufanya mazungumzo na uongozi wa Yanga kuhusu usajili, lakini aliondoka patupu kutokana na kukosekana kwa kiasi hicho cha pesa.
Hata hivyo, Seif alisema wapo mbioni kutafuta kiasi hicho cha pesa ili waweze kukamilisha usajili wa mchezaji huyo haraka iwezekanavyo. Asamoah aliondoka nchini juzi kurejea Ghana. Katika hatua nyingine, kamati ya usajili ya Yanga jana ilitarajiwa kumsainisha mkataba mchezaji Haruna Niyonzima wa APR ya Rwanda mjini Kigali.
Seif alisema jana kuwa, usajili wa mchezaji huyo umechukua muda mrefu kukamilika kutokana na kutoa masharti mazito kwa uongozi wa Yanga.
“Kwa sasa mambo yote yanakwenda vizuri, tumemtuma mjumbe wetu kule Rwanga na tunatarajia Niyonzima atatia saini mkataba wa kuichezea Yanga leo akiwa kwao Kigali,”alisema.
Hata hivyo, Seif hakuwa tayari kutaja kiwango cha pesa walichotumia kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Rwanda kwa madai kuwa, hiyo ni siri ya kamati yake.
Wakati Niyonzima alitarajiwa kumwaga wino jana, klabu hiyo imetangaza kufuta mpango wake wa kumsajili beki wa kimataifa wa Uganda, Godfrey Walusimbi.
Seif amesema wamefikia uamuzi huo kufuatia klabu hiyo kutimiza idadi ya wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za usajili za ligi kuu ya Tanzania Bara.
“Tulikutana na kushauriana na viongozi wa benchi la ufundi na pia kutazama mambo mbalimbali na hatimaye kukubaliana tumuache Walusimbi kwenye usajili wetu,”alisema.
Mbali na Niyonzima na Asamoah, wachezaji wengine wanaotarajiwa kusajiliwa na Yanga msimu ujao ni kipa Yaw Berko wa Ghana, Davies Mwape wa Zambia na Tony Ndolo wa Uganda.
Wachezaji walioachwa na Yanga katika msimu ujao ni pamoja na kiungo, Athumani Idi ‘Chuji’ aliyesajiliwa na Simba, Nelson Kimathi, Nsa Job, Job Ibrahim na Yahya Tumbo.

No comments:

Post a Comment