KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 8, 2011

Asamoah ajipeleka Simba


MSHAMBULIAJI Kenneth Asamoah kutoka Ghana amejipeleka mwenyewe kwa klabu ya Simba ili asajiliwe kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Asamoah, ambaye alikuwa akicheza soka ya kulipwa nchini Serbia, alisajiliwa na Yanga msimu uliopita, lakini alishindwa kuichezea baada ya klabu hiyo kushindwa kumlipia ada ya uhamisho.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, suala la mchezaji huyo limekabidhiwa kwa kamati ya ufundi ya klabu hiyo.
Rage alisema kwa kuwa mchezaji huyo amejipeleka mwenyewe Simba, jukumu lao ni kuangalia uwezo wake na iwapo anafaa kuichezea timu hiyo msimu ujao.
Usajili wa Asamoah uligubikwa na utata mkubwa msimu uliopita baada ya klabu yake ya FK Jagodina ya Serbia kugoma kumpatia uhamisho wa kimataifa (ITC) baada ya Yanga kushindwa kumlipia ada ya uhamisho.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilishindwa kumwidhinisha mchezaji huyo kuichezea Yanga baada ya klabu hiyo na ile ya FK Jagodina kushindwa kufikia makubaliano kuhusu uhamisho wake.
Wakati huo huo, Rage amesema wameshakamilisha taratibu za kumsajili kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka Yanga baada ya kuomba asajiliwe kwa ajili ya msimu ujao.
Rage amesema ujio wa Chuji ni sawa na mtoto aliyerejea nyumbani kwao kutoka safari ndefu ya kutafuta maisha, hivyo hawana kinyongo naye.
“Chuji amerudi nyumbani, hilo halina mjadala, tumeshamalizana naye kila kitu,”alisema Mwenyekiti huyo wa Simba alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 juzi.
Akizungumzia uhamisho wa mshambuliaji Mbwana Samatta, aliyesajiliwa kwa kitita cha sh. milioni 150 na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Rage alisema taratibu zote za uhamisho wake zimeshakamilika.
Rage alisema tayari mchezaji huyo ameshawasili mjini Lubumbashi tayari kwa kuanza kuitumikia timu hiyo. Samatta aliondoka nchini juzi asubuhi kwa ndege ya Shirika la Kenya Airways.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, mkataba kati ya TP Mazembe na mchezaji huyo unaonyesha kuwa, amelipwa dola 50,000 za Marekani (sh. milioni 70) kwa ajili ya uhamisho wake.
Katika mkataba wake huo, Rage alisema Samatta atakuwa akilipwa mshahara wa dola 5,000 za Marekani kwa mwezi (sh. milioni 7.5) na pia kupatiwa matibabu katika hospitali yoyote duniani.
“Ninachoweza kusema ni kwamba Samatta kwa sasa ndiye mwanasoka ghali kuliko wote wa Tanzania wanaocheza nje,”alisema.
Rage alisema pia kuwa, klabu yake inakamilisha mipango ya kuwauza kiungo Patrick Ochan kwa klabu ya TP Mazembe na mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Alisema mipango ya kuwauza wachezaji hao inakwenda vizuri na mara baada ya taratibu kukamilika, watatangaza majina ya wachezaji wapya watakaowasajili kutoka nje kwa ajili ya kuziba mapengo yao.

No comments:

Post a Comment