KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 26, 2011

Simba ni kufa au kupona


Inapambana na Wydad Casablanca keshokutwa
Rage atamba jeshi lake limekamilika kila idara


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika, Simba keshokutwa wanatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi ya raundi ya tatu itakayochezwa mjini Cairo, Misri.
Simba imerejeshwa katika michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kushinda rufani yake dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara, waliilalamikia TP Mazembe kwa kumchezesha mchezaji Janvier Besala Bokungu katika mechi ya awali kati yao kinyume cha kanuni za usajili.
Simba ilidai kuwa, Bokungu hakuwa mchezaji halali wa TP Mazembe kwa vile bado alikuwa na mkataba na klabu yake ya zamani ya Esperance ya Tunisia. Simba ilitolewa katika michuano hiyo na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 6-3.
Mshindi wa pambano hilo, atacheza hatua ya makundi ya ligi hiyo katika kundi B. Timu zingine zilizopangwa kundi hilo ni Al Ahly ya Misri, EST ya Tunisia na Moloudia Club ya Algeria.
Iwapo Simba itatolewa na Wydad Casablanca, italazimika kucheza hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kupambana na DC Motema Pembe ya Congo. Mechi kati ya timu hizo zimepangwa kuchezwa mwezi ujao.
Akihojiwa katika kipindi cha michezo cha Radio One jana, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema Simba ilitarajiwa kuondoka jana usiku kwa ndege kwenda Misri kwa ajili ya mechi hiyo, ikiwa na kikosi cha wachezaji 18 na viongozi kadhaa.
Kwa mujibu wa Rage, wameshafanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mechi hiyo, ikiwa ni pamoja na kupata ushirikiano kutoka ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Misri, ambayo imeiandalia hoteli ya kukaa pamoja na usafiri wa ndani.
Rage alisema Simba itakwenda Misri ikiwa na mashabiki wapatao 1,000 kutoka Tanzania. Alisema wanatarajia kupata mashabiki wengine huko huko Misri, ambako baadhi ya watanzania wanasoma katika vyuo mbalimbali.
Pamoja na kutambia maandalizi waliyoyafanya, Simba itawakosa wachezaji wake Mbwana Samatta na Patrick Ochan, ambao wameuzwa kwa klabu ya TP Mazembe kwa jumla ya kitita cha sh. milioni 300.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilieleza juzi kuwa, CAF imewazuia wachezaji hao kucheza mechi hiyo kwa vile wameshauzwa hivyo kukosa uhalali wa kuichezea Simba.
Simba kupitia TFF ilitaka kufahamu kutoka CAF iwapo inaweza kuwatumia wachezaji hao kwa vile hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) ya kuichezea TP Mazembe bado haijatolewa.
Kwa mujibu wa CAF, wachezaji hao wawili hawawezi kuichezea Simba kwa vile tayari wameshauzwa, hivyo hawana sifa ya kuwa wachezaji wa timu hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 26 (1) ya kanuni za ligi ya mabingwa Afrika.
Pamoja na kanuni kuwazuia wachezaji hao kuichezea Simba, Rage amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuwakabili wapinzani wao na wanakwenda Misri wakiwa na tahadhari kubwa.
Rage alisema pia kuwa, hawana wasiwasi wa mechi hiyo kuchezeshwa na waamuzi kutoka Misri kwa sababu kama timu inao uwezo wa kucheza soka, hawawezi kufanya lolote kuihujumu.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema wanafahamu vyema mbinu, ambazo hufanywa na timu za nchi za ukanda wa kaskazini wakati wa michuano hiyo, hivyo wamejiandaa vyema kukabiliana nazo.
“Hata hao Wamirsi wanafahamu vyema kwamba timu inayokwenda kwao ni tishio barani Afrika, hivyo tunakwenda huko tukiwa tumejiandaa kwa vita,”alisema.
Kocha mpya wa Simba, Moses Basena kutoka Uganda, aliyechukua nafasi ya Patrick Phiri wa Zambia, alisema juzi kuwa, amewaandaa vyema wachezaji wake kisaikolojia na pia kwa mbinu za kukabiliana na wapinzani wao.
Alizitaja baadhi ya mbinu, ambazo amewaelekeza wachezaji wake kuzitumia kuwa ni kuepuka jazba iwapo watabaini mwamuzi anawabeba wapinzani wao ili kukwepa kuonyeshwa kadi nyingi za njano na nyekundu.
“Tunafahamu wazi kwamba Wydad Casablanca ni timu nzuri, lakini hata Simba nayo ni timu nzuri, hivyo mwamuzi wa mwisho ni dakika 90 za uwanjani,”alisema kocha huyo na kusisitiza kuwa, jeshi lake limekamilika katika kila idara.
Alipoulizwa kwa nini kikosi chake hakijacheza mechi za kirafiki kwa ajili ya kujipima nguvu, Basena alisema hofu yake kubwa ilikuwa wachezaji kuumia, hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa timu imebakiwa na wachezaji wachache.
Iwapo timu hizo zitamaliza dakika 90 zikiwa sare, mshindi itabidi apatikane kwa njia ya kupigiana penalti tano tano.
Baadhi ya wachezaji wa Simba wanaotarajiwa kuwemo kwenye safari hiyo ni Emmanuel Okwi, Uhuru Selemani, Rashid Gumbo, Kelvin Yondani, Amri Kiemba, Juma Nyoso, Shija Mkina, Juma Jabu, Nico Nyagawa, Jerry Santo, Abdulrahim Humud, Salum Gila, Mohamed Banka, Salum Aziz na Juma Kaseja.
Swali kubwa wanalojiuliza mashabiki wa soka nchini ni iwapo Simba itaweza kuimudu Wydad Casablanca bila kuwa na mazoezi ya muda mrefu wakati wapinzani wao hao bado wanashiriki katika michuano ya ligi ya Morocco.
Wydad ni timu yenye mafanikio makubwa nchini Morocco, ikiwa imetwaa ubingwa wa nchi hiyo mara 12, sawa na FAR Rabat. Wydad pia imeshika nafasi ya pili mara tisa wakati FAR wameshika nafasi hiyo mara sita.Raja Casablanca, ambayo ni maarufu zaidi nchini kutokana na kupambana na Yanga mwaka 1998, ni ya tatu kwa kuchukua ubingwa wa Morocco mara sita.
Wydad pia imeweka rekodi ya kushinda Kombe la Morocco mara tisa wakati FAR Rabat imelinyakua mara 11. Raja Casablanca ni ya tatu kwa kulitwaa mara sita.
Katika historia yake, Wydad imetwaa ubingwa wa Afrika mara moja mwaka 1992. Mwaka 2002 walitwaa Kombe la Washindi la Afrika na mwaka 1994 walitwaa ubingwa wa nchi za Afrika zenye asili ya kiarabu.
Kikosi cha Wydad kimesheheni nyota wengi wanaocheza katika ligi hiyo na kutoka nje ya nchi. Mmoja wa washambuliaji hao nyota kutoka nje ni Luiz Jeferson Escher kutoka Brazil, ambaye alinunuliwa msimu huu kutoka Kawkab Marrakech ya huko huko Morocco.
Nyota wengine, ambao timu hiyo inajivunia ni pamoja na Jean Louis Paschal Angan na Fabrice N’Guessi, ambaye ni raia kutoka Congo. Angan ni mchezaji wa kimataifa wa Benin. Kwa wachezaji wa nyumbani, Wydad inajivunia nyota wake, Youness Mankari. Kocha Mkuu wa timu hiyo ni Fakhreddine Rahji.

No comments:

Post a Comment