LOS ANGELES, Marekani
JADEN Smith ametajwa kuwa ndiye mcheza filamu mtoto anayelipwa fedha nyingi zaidi Hollywood.
Mtoto huyo wa mwanamuziki na mcheza sinema, Will Smith wa Marekani, ameweka rekodi hiyo baada ya kulipwa dola milioni mbili kutokana na kuwa mwigizaji mkuu wa filamu ya The Karate Kid.
Licha ya kuwa na umri wa miaka 13, Jaden amelipwa kiasi hicho cha fedha kutokana na uigizaji wake mzuri na pia mafanikio ya filamu hiyo sokoni.
Awali, Jaden alilipwa dola milioni moja kama malipo ya mwanzo kwa ajili ya kucheza filamu hiyo.
Filamu hiyo ilikuwa ya tatu kwa Jaden, lakini ni ya kwanza kucheza akiwa mwigizaji mkuu, akishirikiana na Jackie Chan.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao, Jaden atakuwa akilipwa bonasi kila filamu hiyo itakapokuwa ikipata mauzo mazuri sokoni.
Gharama za kutengeneza filamu hiyo ya The Karate Kid zinakadiriwa kufika dola milioni 150 wakati Jaden alilipwa bonasi ya dola milioni mbili.
Mbali na kujihusisha na fani ya filamu, Jaden pia ni mwanamuziki. Moja ya vibao vilivyompatia umaarufu ni ‘Never Say Never’, alichokiimba na Justin Bieber.
Jaden alianza kucheza filamu akiwa na umri wa miaka 10. Filamu ya The Karate Kid iliandaliwa mwaka 2010 alipokuwa na umri wa miaka 12.
Filamu yake ya kwanza inajulikana kwa jina la The Pursuit of Happyness, aliyoshiriki kucheza sehemu ndogo akiwa na baba yake, Will Smith.
Dada wa kijana huyo, Willow pia ni mwanamuziki, ambaye kibao chake cha Whip My Hair kimeshika nafasi ya pili kwenye chati ya ubora nchini Uingereza.
Willow pia ameshiriki kucheza filamu kadhaa, ikiwemo Iam Legend. Alicheza filamu hiyo kwa kushirikiana na baba yake, Will.
Watoto hao wawili wamepata baraka za kujitosa kwenye fani hiyo kutoka kwa wazazi wao, Will na mama yao, Jada Pinkett Smith.
No comments:
Post a Comment