'
Thursday, May 26, 2011
Yanga kuilipa CECAFA mil. 52/-?
KLABU ya Yanga imesema ipo tayari kulipa faini ya dola 35,000 za Marekani (sh. milioni 52) ilizotozwa mwaka 2008 na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Celestine alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wapo tayari kulipa faini hiyo ili waweze kushiriki michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu.
CECAFA imeamua kuhamishia michuano hiyo nchini Tanzania kutoka Sudan, kufuatia mapigano yaliyozuka nchini humo kati ya majeshi ya Sudan na Sudan Kusini.
Kwa mujibu wa kanuni za baraza hilo, nchi mwenyeji huwakilishwa na timu mbili, bingwa wa ligi na mshindi wa pili. Simba itashiriki michuano hiyo ikiwa bingwa wa ligi ya mwaka jana wakati Yanga ilishika nafasi ya pili.
Yanga ilitozwa faini hiyo na CECAFA baada ya kugoma kucheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu wa michuano hiyo kati yake na Simba mwaka 2008 mjini Dar es Salaam, ikitaka ilipwe dola 50,000.
Mbali na kutozwa faini, Yanga pia ilifungiwa kushiriki katika michuano hiyo kwa miaka mitatu. Adhabu hiyo inatarajiwa kumalizika mwaka huu.
“Tunataka kushiriki katika michuano ijayo ya Kombe la Kagame, ambayo pia tutaitumia kukipima kikosi chetu kabla ya mashindano ya klabu bingwa Afrika,”alisema Mwesigwa.
“Tunataka kulimaliza sakata hili. Kwa sasa, tunajadiliana na viongozi wa CECAFA kwa lengo la kulipa faini hiyo. Tunaguswa sana kwa sababu ni pesa nyingi, lakini hatuna jinsi,”aliongeza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment