SWALI: Hongera sana kwa kuiwezesha timu ya mkoa wa Mbeya kutwaa Kombe la Taifa mwaka huu na pia wewe binafsi kunyakua tuzo ya kocha bora. Unaweza kutueleza nini siri ya mafanikio hayo?
JIBU: Asante sana, nashukuru kwa pongezi zako. Kwa kweli hakuna jipya, siri ya mafanikio ya timu yangu ni kuwepo mshikamano miongoni mwa viongozi, makocha, wachezaji na wadau wa soka waliokuwa wanatuunga mkono.
Mbali na hayo, napenda kuwashukuru viongozi wa mkoa wetu na hasa mkuu wa mkoa kwa kutupa ushirikiano wa kutosha kuanzia hatua ya mwanzo hadi mwisho wa mashindano hayo.
Kwa kweli nitakuwa mkosefu wa fadhila endapo sinyawapongeza wachezaji wangu kwa kunisikiliza kwa makini muda wote wa mashindano na kufuata maelekezo yangu. Pia nawapongeza kwa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu muda wote wa mashindano.
Timu ya mkoa wa Mbeya safari hii ilikuwa na wachezaji wengi wenye uwezo na walikuwa na dhamira halisi ya kuhakikisha wanaibuka na taji hilo. Licha ya kupata wakati mgumu kutoka kwa wapinzani wetu, kwa kweli mashindano yalikuwa na ushindani mkubwa.
SWALI: Umejifunza nini kipya kutokana na mashindano ya mwaka huu?
JIBU: Nimejifunza vitu vingi. Cha kwanza kabisa, nimegundua kwamba Tanzania inavyo vipaji vingi, lakini havipati nafasi ya kuonekana. Wachezaji, ambao walicheza katika mashindano yale, walikuwa katika viwango vya hali ya juu na waliweza kutimiza malengo yao.
Jambo la pili nililojifunza ni kwamba, nimegundua katika mashindano haya, wachezaji wengi walikuwa na nidhamu ya hali ya juu na ndio maana kulikuwa hakuna taarifa za mambo ya ajabu ajabu kama tulivyokuwa tumezoea kuona na kusikia.
Katika mashindano hayo miaka ya nyuma, ilikuwa kitu cha kawaida kuona ama kusikia matukio ya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa wachezaji, lakini mwaka huu, hayo mambo hayakuwepo kabisa.
Vilevile nimejifunza kuwa, kuwepo kwa uwazi kumesaidia wachezaji wengi wenye vipaji kupata ofa ya kwenda kujiunga na timu zitakazoshiriki michuano ya ligi kuu msimu ujao. Haya ni mafanikio makubwa.
Mambo yote yametokana na kupatikana mafanikio kwenye mashindano hayo, ambayo napenda kukiri kwamba yalikuwa magumu kutokana na vijana wengi kupania kuibuka na zawadi za ushindi wa kwanza.
Nadhani kuwepo kwa zawadi kubwa ya pesa kwa washindi wa kwanza, kulichangia kuwepo kwa ushindani. Timu nyingi zilicheza soka ya kiwango cha juu, lakini bahati nzuri ni kwamba ulikuwa wakati wetu wa kuibuka mabingwa.
SWALI: Ni kasoro zipi ulizozibaini katika mashindano ya mwaka huu?
JIBU: Kasoro zilikuwepo chache, pengine kubwa ilikuwa baadhi ya waamuzi kushindwa kutafsiri vyema sheria 17 za soka na wengine kushindwa kwenda na kasi ya mchezo.
Nalipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa uamuzi wake wa kutoa nafasi kwa wachezaji wa timu za madaraja ya chini kushiriki mashindano hayo. Nadhani ni vyema utaratibu huu uwe endelevu.
Kuwepo kwa wachezaji wachache wa ligi kuu katika mashindano hayo, kunaweza kuongeza ushindani zaidi na pia kutoa nafasi kwa vijana chipukizi waliopo madaraja ya chini kuonyesha vipaji vyao.
SWALI: Unafikiri nini kifanyike ili wachezaji chipukizi waweze kupata nafasi kubwa zaidi ya kuonyesha uwezo wao?
JIBU: Nadhani ni vyema tubuni zaidi mipango ama taratibu za kuanzisha mashindano mengi kwa lengo la kusaka na kuibua vipaji vya vijana. Utaratibu huu uanzie katika ngazi ya mkoa. Pia TFF isilegeze buti kuhusu uamuzi wake wa kuzuia wachezaji wengi wa ligi kuu kushiriki katika mashindano haya.
Vilevile napenda kutoa mwito kwa viongozi wa vyama vya mikoa kujaribu kuangalia uwezekano wa kuziandaa timu zao mapema ili kusaka wachezaji katika mashindano mbalimbali ya ndani ya mikoa yao.
SWALI: Una ushauri gani kwa TFF kuhusu kuyaboresha zaidi mashindano hayo?
JIBU: Nawaomba viongozi wa TFF kuangalia uwezekano wa kuongeza nguvu zaidi katika maandalizi ya mashindano ya vijana ili wachezaji waweze kupatikana kabla ya kuanza mashindano ya Kombe la Taifa.
Ushindani pia unaweza kuongezwa kwa viongozi wa TFF kupitia kwa wadhamini kuboresha zaidi zawadi za wafungaji,wachezaji bora na makipa bora ili ushindani uzidi kuongezeka.
Kila mchezaji kwa sasa anapenda kuboresha maisha yake kupitia mchezo huo, kwa maana hiyo kama zawadi zitaongezwa, kuna uwezekano mkubwa ushindani utaongezeka na pengine wachezaji wengi kuvutiwa zaidi na mashindano hayo.
Nina hakika kuwa, ushindano katika michuano ya Kombe la Taifa ukiwa mkubwa, itakuwa rahisi pia kwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen kupata wachezaji wengi zaidi kwenye timu yake.
SWALI: Una ushauri gani kwa serikali kuhusu kuongeza kasi ya kukua kwa kiwango cha soka hapa nchini?
JIBU: Ushauri wangu kwa serikali ni kwamba wakati umefika kwa viongozi wake kuangalia uwezekano wa kuwafundisha walimu wa michezo kuanzia katika ngazi za shule ya msingi, sheria za soka ili vipaji vianze kufunzwa tangu vijana wakiwa wadogo.
Tukifanya hivyo, nina hakika tutaweza kutimiza malengo ya kukuza mchezo huo. Pia naiomba serikali ijaribu kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi katika vifaa vya michezo.
Iwapo serikali itafanya hivyo, nina hakika vijana wengi wataweza kumudu gharama za kununua vifaa vya michezo na hivyo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika michezo mbalimbali.
Pia nawaomba wamiliki wa gym kupunguza gharama za kufanya mazoezi ili vijana wengi waweze kuzimudu na hivyo kuiweka miili yao iwe fiti muda wote. Hii pia itawasaidia watu wazima kupunguza uwezekano wa kuugua baadhi ya magonjwa kama vile sukari na shinikizo la damu.
Mwisho naipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kurejesha michezo katika shule za msingi kwa sababu huko ndiko kwenye vipaji na lazima viongozi wamuunge mkono na mafanikio yake yataonekana.
No comments:
Post a Comment