Na Gule Mandago, DSJ
KLABU ya Simba imetangaza kuwatema wachezaji wake saba wa zamani, ambao itawauza kwa mkopo kwa klabu zingine katika msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Simba iliwasilisha orodha ya wachezaji hao kwa shirikisho hilo juzi.
Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Aziz Gila, Meshack Abel, David Naftali, Juma Jabu na Haruna Shamte.
Angetile alisema Simba imeamua kuwauza wachezaji hao kwa mkopo kwa vile bado wana mikataba na klabu hiyo.
Alisema Simba pia imetangaza kuwaacha Rashid Gumbo, Hillary Echessa na Emmanuel Okwi kutokana na mikataba yao kumalizika.Tayari Gumbo ameshasajiliwa na Yanga.
Katibu Mkuu huyowa TFF pia alisema, Simba imewauza wachezaji wake wengine watatu, Mbwana Samatta, Patrick Ochan na Abdulrahim Humud kwa klabu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Azam FC.
Barua ya Simba iliyotumwa TFF imeeleza kuwa, klabu hiyo haitarajii kuwaacha wachezaji wake wengine walioichezea timu hiyo msimu uliopita.
Baadhi ya wachezaji hao ni makipa Juma Kaseja na Ally Mustapha Barthez, Salum Kanoni, Kelvin Yondan, Juma Nyoso, Mohamed Banka, Shija Mkina, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Nico Nyagawa.
Wakati huo huo, viongozi wa klabu ya Simba wameanza kufanya mazungumzo na uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa ajili ya kumuombea ruhusa ya usajili kiungo, Mwinyi Kazimoto. Mbali na Kazimoto, Simba pia imeanza kufuatilia uhamisho wa wachezaji Salum Machaku na Obadia Mungusa kwa klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Simba pia huenda ikamrejesha kundini, mshambuliaji wake wa zamani, Ulimboka Mwakingwe, ambaye aliuzwa kwa mkopo kwa timu ya Majimaji ya Songea.
Kuna habari pia kuwa, Simba inafanya mipango ya kuwasajili wachezaji wawili kutoka nchi za Nigeria na Ghana. Hata hivyo, majina ya wachezaji hao bado hayajawekwa wazi.
No comments:
Post a Comment