'
Wednesday, June 15, 2011
SAMATTA: Lazima niwapangue mastaa wa TP Mazembe
SWALI: Hongera kwa kufanikiwa kuingia mkataba wa kuichezea timu ya TP Mazembe. Je, unaweza kueleza nini siri ya mafanikio hayo?
JIBU: Asante, nashukuru sana. Siri kubwa ya mafanikio yangu ni kuwa na msimamo na kuzingatia mafunzo ya makocha, ambao wamekuwa wakinifundisha na mimi kufanyiakazi .
Mbali na hilo, malengo yangu kwa sasa ni kuonyesha uwezo zaidi wa kucheza soka ndani ya timu hiyo ili hatimaye siku zijazo niweze kwenda kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya.
Hilo jambo lipo kwenye mawazo yangu siku nyingi, hasa ninapowaona wachezaji kama Nizar Khalfan, Henry Joseph na Danny Mrwanda wanavyopata maendeleo katika klabu zao kupitia mchezo wa soka.
Lakini napenda kuweka wazi kuwa, safari yangu ya mafanikio ndio kwanza imeanza, hivyo nitahakikisha nachuana vikali na mastaa wa TP Mazembe ili niweze kupata namba katika kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, najua wazi kwamba itanibidi nifanyekazi ya ziada ili kuhakikisha lengo la kuwapiku wakali hao linatimia. Nitalazimika kuonyesha uwezo wangu ili niweze kupata ulaji huko ulaya. Sioni sababu ya kushindwa kufanya hivyo.
Lakini napenda kueleza wazi kuwa, tangu nimeanza kucheza soka katika timu za mtaani, Amani nimekuwa nikifanya jitihada kubwa kujiendeleza. Pia nimewahi kuchezea timu za Mbagala Market ,TMK United na African Lyon kabla ya kutua Simba.
SWALI: Baada ya kujiunga na TP Mazembe, umegundua tofauti gani kati ya soka la hapa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo?
JIBU: Tofauti ipo, lakini sio kubwa. Lakini lazima nikiri kwamba, wenzetu wamejipanga katika kila idara kwenye klabu na kila moja inafanyakazi yake bila ya kuwepo ubabaishaji.
Ukiangalia viongozi wa klabu hiyo, utaona kuwa wanafanyakazi kwa ushirikiano mkubwa na kuwajali zaidi wachezaji ili kuhakikisha wanakuwa fiti na malengo yao yanatimia.
Mbali na hayo, karibu wachezaji wote kila mmoja anatambua kwamba yupo pale kwa ajili ya kucheza soka na kuipa mafanikio klabu hiyo, hivyo wanajali kufanya mazoezi kwa muda mwingi ili kuhakikisha wanakuwa fiti.
Vilevile klabu imeweza kujitosheleza kwa vifaa vya mazoezi kama vile gym na vinginevyo. Vifaa vyote hivyo vimepewa umuhimu kwa lengo la kuwaweka wachezaji fiti.
Binafsi nimepata morari kubwa ya kucheza soka kutokana na hali niliyoikuta TP Mazembe. Nimekuwa nikijituma sana kwenye mazoezi ili niweze kuwa fiti na kupangwa kwenye kikosi cha kwanza.
SWALI:Una maoni gani kuhusu timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 23, ambayo inatarajiwa kucheza na Nigeria mwishoni mwa wiki hii?
JIBU: Nina imani kubwa na kikosi cha timu hiyo kwani kipo fiti kutokana na mazoezi, ambayo tumekuwa tukipewa na kocha wetu Jamhuri Kihwelu.
Matumaini yetu makubwa ni kwamba tutashinda mechi hiyo kutokana na wachezaji wote kuwa na morari kubwa, hasa ikizingatiwa kuwepo kwa changamoto ya zawadi, ambayo tumepewa hivi karibuni na mfanyabiashara Azim Dewji.
Vilevile napenda kulipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)kwa kuipa matunzo mazuri timu hiyo kama ilivyo kwa timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars.
SWALI: Unaahidi nini kuhusu mchezo huo wa marudiano, ambao ni muhimu kwa timu ya vijana kushinda?
JIBU: Nawaomba Watanzania wote kila mmoja kivyake, watuombee dua ili tuweze kushinda mchezo huo muhimu na kusonga mbele katika michuano ya kusaka kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012 kule Uingereza.
SWALI: Wewe ni mtoto wa ngapi katika familia yenu na katika ukoo wenu kuna mtu yeyote ambaye amewahi kucheza soka?
JIBU: Mimi ni mtoto wa mwisho katika familia ya mzee Ally Samatta, ambaye amejaliwa kupata watoto sita.
Baba yangu aliwahi kucheza soka katika timu ya Pamba ya mkoani Mbeya na watoto wote sita waliweza kufuata nyayo za baba yetu.
Lakini mimi na kaka yangu, Mohamed ambaye yupo African Lyon bado tunaendelea kucheza soka. Mimi nilizaliwa mwaka 1992 katika hospitali ya Bombo mkoani Tanga. Nimesoma shule ya msingi Mbeya kabla ya baba kuacha kazi ya upolisi na kuamua kurudi jijini Dar es Salaam na familia yake.
Nilimaliza masomo ya shule ya awali mwaka 2003 kule Mbagala Rangitatu na kujiunga na shule ya sekondari ya Thaqhalain. Nilimaliza elimu ya sekondari mwaka 2008 na muda wote huo nilikuwa nikicheza soka baada ya masomo.
SWALI: Una maoni gani, ambayo ungependa kuyatoa kwa viongozi wa serikali kuhusu maendeleo ya michezo hapa nchini?
JIBU: Kwanza kabisa napenda kuipongeza serikali, inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kurejesha michezo katika shule za msingi na sekondari.
Najua wachezaji wengi wapo katika shule mbalimbali, lakini hawapati nafasi ya kuonekana. Ni jambo zuri kuona kuwa, Chuo cha Michezo kilichopo Malya mkoani Mwanza kimeanza kutoa mafunzo ya michezo kwa walimu wa shule za sekondari. Jambo la msingi ni kwa chuo hicho kupatiwa wakufunzi wazuri zaidi.
Iwapo chuo hicho kitapewa kipaumbele, nina hakika katika siku zijazo tutakuwa na wanamichezo wazuri pamoja na makocha wazuri wa michezo mbalimbali kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Pia napenda kuwapa somo wachezaji wenzangu kuwa, tuongeze bidii ya kujituma katika mazoezi ili tuwe fiti na kufanikiwa katika maisha yetu kupitia soka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment